1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAsia

China yafanya majaribio ya kombora la masafa marefu

Hawa Bihoga
25 Septemba 2024

China imerusha kombora la majaribio la masafa marefu katika eneo la bahari ya Pasifiki. Tukio hilo limezusha wasiwasi wa kiusalama katika eneo hilo ambapo jirani yake Japan imesema haikupewa taarifa ya majaribio hayo.

https://p.dw.com/p/4l3lf
China ikionesha zana makombora yake ya masafa marefu.
China ikionesha zana makombora yake ya masafa marefu.Picha: Tang Yanjun/China News Service/picture alliance

Wizara ya Ulinzi Beijing imesema katika taarifa yake kwamba kombora hilo aina ya ICBM ambalo kichwa chake sio halisi lilirushwa kwenye kina kirefu katika bahari ya Pasifiki.

Majaribio hayo ya Kikosi cha Roketi cha Jeshi la China ulikuwa ni sehemu ya mafunzo ya kawaida ya kila mwaka, ambayo china inasema yamezingatia sheria za kimataifa na hayakuelekezwa dhidi ya nchi yoyote.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi China Zhang Xiaogang katika taarifa yake amesema majaribio ya kombora hilo yalifanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na kombora hilo kuanguka katika maeneo ya bahari ya Pasifiki ambayo yalitarajiwa.

"Kikosi cha makombora cha jeshi la China kimerusha kombora la masafa marefu lililobeba kichwa cha kivita kisicho halisi kuelekea bahari ya Pasifiki leo Septemba 25 na kombora hilo limeanguka katika eneo la bahari lililotarajiwa."

Japan ikizungumzia majaribio hayo imesema haikupata taarifa kutoka China, huku msemaji wa serikali akiongeza kwamba kujiimarisha kwa jeshi la China kunatia wasiwasi.

Soma pia:Korea Kaskazini yafanya majaribio ya makombora mapya ya masafa mafupi

New Zealand pia imesema kurushwa kwa kombora hilo ambalo lilitua upande wa Kusini mwa Pasifiki hakukubaliki na imesema itafanya mashauriano zaidi na washirika wa Pasifiki.

Haijabainika, ni mara ngapi China imefanya majaribio kama hayo, lakini ikumbukwe kwamba mnamo mwaka 1980 China ilirusha kombora la masafa marefu katika eneo la bahari ya Pasifiki kusini.

Ramani iliyochapishwa kwa wakati huo na magazeti ya nchini humo ilionesha eneo la pembe tatu lililolengwa ilionesha visiwa kadhaa ikiwemo Solomon, Nauru pamoja na Samoa ya magharibi.

Maendeleo ya China katika nyuklia

Beijing imekuwa ikipiga hatua za haraka katika maendeleo yake ya nyuklia na imeongeza bajeti yake katika sekta ya ulinzi katika miaka ya hivi karibuni, mwaka uliopita Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilionya juu ya China kuongeza kasi katika utengenezaji wa silaha kuliko ilivyotarajiwa Washington.

Kombora lililofyatuliwa.
Kombora lililofyatuliwa.Picha: South Korea Defense Ministry/AP Photo/picture alliance

Hadi kufikia mwaka uliopita China ilimiliki vichwa 500 vya nyuklia na kuna uwezekano wa silaha hizo kuongezeka mpaka ifikapo mwaka 2030, kulingana na Marekani.

Mnamo mwezi Novemba Marekani na China zilifanya mazungumzo ya nadra kuhusu udhibiti wa silaha za nyuklia, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza hali ya kutoaminiana kabla ya mkutano wa kilele kati ya viongozi Joe Biden na Xi Jinping.

Soma pia:Dunia yakaribisha uamuzi wa Korea Kaskazini kusitisha majaribio ya nyuklia

Hata hivyo mwezi Julai, Beijing ilisema ilisitisha mazungumzo na Marekani juu ya kutoeneza silaha za nyuklia na udhibiti wa silaha ili kukabiliana na mauzo ya silaha ya Washington kwa Taiwan.

Mwezi huu, maafisa waandamizi wa kijeshi kutoka China na Marekani walifanya mazungumzo "ya kina" kama sehemu ya jitihada za mamlaka ili kuepuka mivutano mikubwa inayozidi kufukuta.