Urusi na China zapinga mbinyo zaidi dhidi ya Korea Kaskazini
27 Mei 2022Azimio hilo liliwasilishwa na Marekani limepata uungwaji mkono wa wanachama 13 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kupingwa na China pamoja na Urusi. Kuelekea kura ya siku ya Alhamis, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield alisema kwamba azimio hilo, "litazuia uwezo wa Korea Kaskazini wa kuendeleza silaha haramu za maangamizi makubwa pamoja na mpango wake wa makombora ya masafa marefu, kurahisisha utekelezwaji wa vikwazo na kuwezesha usambazaji wa misaada ya kiutu.
China, mshirika wa karibu wa Korea Kaskazini na Urusi, ambayo uhusiano wake na nchi za magharibi umedhoofika zaidi kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine, imesema kwamba ingependelea zaidi tamko lisilofungamana badala ya azimio jipya la vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini.China na Urusi zazuia vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa Zhang Jun amesema kwamba Marekani "haipaswi kutilia mkazo upande mmoja juu ya utekelezwaji wa vikwazo", lakini pia ifanyie kazi kuhamasisha suluhisho la kisiasa. Ameonya kwamba vikwazo hivyo vitazidisha athari za kibinadaamu kwa Korea Kaskazini. Zhang ameongeza kwamba Marekani ilitaka azimio hilo lishindwe kupita ili iweze "kueneza moto wa vita" kama sehemu ya juhudi ya kuishinikiza China.Ni kwa nini Pyongyang ilidanganya kuhusu jaribio la kombora?
Naye Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia ameishutumu Marekani kwa kupuuza wito wa Korea Kaskazini wa kusitisha "shughuli za uadui". Ameongeza kuwa Marekani na washirika wake wanaonekana kutokuwa na suluhisho na badala yake kuanzisha vikwazo vipya.
"Tungependa kusisitiza tena kwamba Urusi inapinga shughuli zozote za kijeshi zinazotishia usalama wa Rasi ya Korea na Kaskazini Mashariki mwa Asia. Hata hivyo, suala la usalama ambalo linagusa nchi yetu moja kwa moja haliwezi kushughulikiwa kwa njia za kale za vikwazo, ambazo husababisha madhara makubwa. Tuna hakika kwamba utafutaji wa suluhu za kidiplomasia ndiyo njia pekee ya kufikia suluhu ya amani kwenye Rasi ya Korea Kaskazini na kuunda mifumo imara ya usalama Kaskazini Mashariki mwa Asia.”
Siku ya Jumatano, Korea Kaskazini ilifyatua makombora matatu ya masafa marefu kwa mfululizo katika eneo la wazi la bahari. Kumekuwa na ishara zinazozidi kuongezeka kwamba nchi hiyo inajiandaa kwa ajili ya jaribio la nyukilia. Majaribio hayo ya hivi karibuni ya Korea Kaskazini yanafanyika katika wakati ambao wasiwasi wa usalama umezidi kuongezeka katika kanda hiyo. Jaribio hilo la Jumatano ni la 17 kufanywa na Pyongyang ndani ya mwaka huu. Utawala wa Rais Joe Biden umesema mara kwa mara kwamba uko tayari kwa mazungumzo na Korea Kaskazini bila masharti.