COP15: Bado hakujafikiwa mafanikio makubwa
13 Desemba 2022Maoni ya wengi yanabaini kuwa mazungumzo hayo yatakuwa magumu zaidi siku ya Alhamisi, wakati mawaziri wa mazingira kutoka kwa wanachama 196 wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa bioanuawi (CBD), watakapochukua nafasi kutoka kwa wajumbe wao huko Montreal.
Lakini uwezekano wa kufikia makubaliano mnamo Desemba 19 kuhusu "mkataba wa kuheshimisha mazingira", unaojumuisha malengo 20 ya kukomesha uharibifu wa maji, misitu na viumbe hai ifikapo mwishoni mwa muongo huu, utakuwa hafifu ikiwa rasimu ya makubaliano hayo itasalia kama ilivyo sasa.
Soma zaidi: COP15: Bioanuwai ni nini na kwa nini ni muhimu sana?
Licha ya wajumbe 5,000 kujadiliana kwa muda mrefu tangu Desemba 3, rasimu hiyo bado haijakamilika huku mada kadhaa zikiwa bado mezani. Hadi sasa, malengo matano pekee kati ya 22 au 23 yaliyotarajiwa ndiyo yaliyopatiwa ufumbuzi.
Alfred DeGemmis, afisa mkuu katika Jumuiya ya Kuhifadhi Wanyamapori (WCS) amesema kuwa wajumbe wa Serikali wanapiga hatua, lakini si kwa kasi ya kutosha ili kufikia kuandaa rasimu kamili kabla ya kuwasili kwa mawaziri.
Soma zaidi:COP15: Kampuni zatakiwa kutangaza madhara yao kwa mazingira
Muda unatutupa mkono: aina ya wanyama milioni moja iko hatarini kutoweka, theluthi moja ya ardhi imeharibiwa vibaya, rutuba ya udongo na maji safi viko hatarini, huku bahari zikitishiwa na uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa.
Marco Lambertini, mkuu wa shirika la kimataifa la kulinda wanyamapori WWF, amesema bado wako mbali kufikia rasimu hiyo, lakini wanakaribia kuikamilisha. Ameongeza kuwa, tangu kuanza kwa mazungumzo hayo, ameshuhudia juhudi endelevu.
Tatizo la ufadhili kwa mataifa yanayoendelea
Kwa upande wake Sebastien Treyer, mkurugenzi mkuu wa taasisi ya utafiti ya IDDRI amesema kumekuwa kukiibuka msukumo wa nchi za Kusini mwa dunia, kutaja kuwa hazitakubali kudiriki katika makubaliano yoyote bila ya kupewa ufadhili unaostahiki.
Soma zaidi: Mkutano wa Bayoanuwai COP15 wafunguliwa Canada
Siku ya Jumamosi, Brazil ilisisitiza, kwa niaba ya bara la Afrika na nchi nyingine 14 zikiwemo India na Indonesia, maombi yao ya "ruzuku ya kifedha ya angalau dola bilioni 100 kwa mwaka au asilimia moja ya Pato la dunia hadi ifikapo mwaka 2030."
Nchi tajiri zimekuwa zikionyesha kuwa ongezeko hilo halitowezekana wakati misaada yake iliyotengwa kwa ajili ya bioanuwai mnamo mwaka 2020 ilifikia tu dola bilioni 10.
Soma zaidi: Wanaharakati wataka miito yao kulinda bayoanuwai isikizwe
Mjumbe wa Ufaransa kwenye mkutano huo wa COP15, Sylvie Lemmet, ameonya kuwa, kuzungumzia ghafla tu kuhusu kitita cha bilioni 100 kunayafifisha malengo ya mazungumzo hayo hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa msaada uliyofikiwa ni bilioni 10 huku nchi tajiri zikiwa pia zimeahidi kuongeza misaada ya maendeleo katika muongo mmoja uliopita.
Umoja wa Ulaya pia unapinga kuundwa kwa hazina mpya ya kimataifa ya bioanuwai, jambo ambalo litakuwa kipaumbele kwa nchi kadhaa kwenye mkutano mwengine wa COP16 utakaofanyika mwaka 2024 nchini Uturuki.