COP27: Nishati mbadala kusaidia hali ya hewa, usalama
10 Novemba 2022Akizungumza Alhamisi katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi COP27, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati Mbadala, Francesco La Camera amesema soko kwa sasa linawalazimisha wote, lakini wanapaswa kuhakikisha nishati mbadala zinaendelea kukua haraka na ameonya kwamba kasi inahitaji kuongezeka maradufu ili kuzuia janga la hali ya hewa.
Amesema vita vya Ukraine vimesababisha mdororo mkubwa wa usambazaji wa nishati na kupanda kwa bei ya mafuta na gesi ambako kumezilazimisha hasa nchi za Ulaya kutafuta haraka wasambazaji wapya wakati zikielekea katika majira ya baridi.
Hakikisho la uhuru wa nishati
La Camera amesema kwa muda mfupi hilo litakuwa na athari, lakini katika muda wa kati na mrefu, hakuna njia nyingine zaidi ya kuharakisha katika kuachana na gesi ya kaboni kwa sababu nishati mbadala sio tu nzuri kwa ajili ya mazingira, ajira na pato la ndani la taifa, lakini pia ni njia halisi ya kuhakikisha uhuru wa nishati.
''Nchini Marekani viwanda vya makaa ya mawe vinafungwa. Kwa hiyo, soko tayari linasema wazi kwamba tunaelekea kwenye mfumo mpya wa nishati kwa kutegemea nishati mbadala na inayojazwa na haidrojeni, hasa haidrojeni ya kijani na endelevu. Hakuna mtu anayeweza kuzuia maendeleo haya,'' alifafanua La Camera.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg pia ameangazia kipengele cha kimkakati cha kuachana na kuitegemea Urusi na wasambazaji wengine wa mafuta na gesi kwa kutumia nishati mbadala ambazo ni safi na salama. Amesema hatua ya Urusi kuitumia nishati kama silaha ni ukumbusho tosha kwamba wanahitaji kuhama kutoka kuwa tegemezi wa nishati ya mafuta na kuanza kutumia nishati mbadala kwa sababu hilo litawafanya wasiitegemee sana gesi na mafuta ya Urusi.
Wabunge wa chama cha Democratic nchini Marekani wanaohudhuria mkutano wa COP27 wameelezea wasiwasi wao kwamba ushindi wa Republican katika uchaguzi wa bunge wa katikati ya muhula unaweza kusababisha matatizo katika juhudi za Marekani za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Biden na sera za mazingira
Serikali ya chama cha Democratic ya Rais Joe Biden, ina matumaini kwamba Marekani ambayo ni mtoaji wa pili duniani wa gesi chafu ya kaboni ikiwa nyuma ya China, inaweza kuwa kiongozi wa dunia katika kupunguza utoaji wa gesi chafu, lakini inakabiliwa na upinzani wa kisiasa kutoka kwa wanachama wa Republican ambao wanasema sera zake za mazingira hazifai.
Ama kwa upande mwingine, wataalamu wa mazingira wanasema kuwa bara la Afrika ambako mkutano wa COP unafanyika kwa mwaka huu, lina uwezo mkubwa wa kutumia nishati mbadala, hasa nishati ya jua, lakini hadi sasa iko nyuma. Ripoti iliyotolewa na watafiti wa shirika la BloombergNEF, imeeleza kuwa uwekezaji katika nishati mbadala Afrika umepungua na bara hilo limepata asilimia 0.6 pekee ya uwekezaji wa kimataifa katika sekta hiyo. Kwa mujibu wa wataalamu hao, Afrika ina uwezo wa kuzalisha mara 1,000 ya umeme na nishati wanayohitaji.
(AFP, Reuters)