DRC na MONUSCO wahitaji mkakati dhidi ya waasi
21 Oktoba 2014Hiyo ilikuwa baada ya mauaji ya kikatili linalodaiwa kuyafanya dhidi ya raia mashariki mwa Kongo. Je, hii ina maana kundi hilo halikutokomezwa kama ilivyodaiwa awali? Na je, upo mkakati mwafaka dhidi ya waasi mashariki mwa Kongo?
Mwandishi wa DW Maja Braun ameyaangazia masuala hayo katika mahojiano aliyofanya na Thierry Vircoulon, mtaalamu wa masuala ya Kongo kutoka Shirika la Kimataifa linaloshughulikia migogoro, ICG.
Katika mahojiano hayo, mtaalamu huyo kutoka ICG Thierry Vircoulon anasema hakuna shaka yoyote kwamba mauaji ya Ijumaa iliyopita ambayo yalilenga raia, yalikuwa ni kitendo cha ulipizaji kisasi kilichofanya na kundi la ADF.
Anasema kwa uzoefu wake, mtindo uliotumiwa na ADF kuwauwa raia hao kwa kuwakata kwa mapanga ulilenga kueneza hofu miongoni mwa wahanga, kama onyo kwamba iwapo wataipinga watakufa kifo kibaya.
Madhumuni ya ADF ndani ya Kongo
Vircoulon amesema madhumuni ya ADF katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Vircoulon amesema malengo ya ADF ni kuipindua serikali ya Uganda na sio serikali ya Kinshasa, na kwamba kwa muda wa miaka 20 limekuwa likijihifadhi katika milima ya Rwenzori iliyo kwenye mpaka baina ya Kongo na Uganda. Kulingana na maelezo ya mtaalamu huyo, operesheni za hivi karibuni dhidi ya kundi hilo zililifukuza kutoka kwenye milima hiyo, na kuwalazimisha kukimbilia ndani zaidi ya Kongo.
Amesema ripoti kwamba kundi hilo lilikuwa limeshindwa hayakuwa sahihi, kwa sababu liliweza kukimbia na kukita kambi mahali pengine. Kwa makisio yake, kundi hilo kwa sasa linabakiwa na wapiganaji takribani 400.
MONUSCO imekosa mkakati?
Kufuatia mauaji hayo ya Ijumaa iliyopita dhidi ya raia, mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO, Martin Kobler alitoa salamu zake za rambi rambi, na kuahidi ushirikiano zaidi na jeshi la serikali katika kulitokomeza kundi la ADF. Hata hivyo, Vircoulon amesema MONUSCO imefanya makosa kimkakati.
''Mbinu zinazotumiwa na MONUSCO pamoja na jeshi la Kongo, za kushambulia kwa mabomu ngome za waasi hao, haziwezi kulivunja kundi hilo isipokuwa kama yangeweza kuwauwa wapiganaji wote pamoja na viongozi wao. Kilichofanyika ni kuwatawanya tu wapiganaji wa kundi hilo, na kinachodhihirika ni kwamba wamejikusanya upya na kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi. Hali inazusha wasiwasi juu ya iwapo kweli MONUSCO na jeshi la Kongo wanao mkakati wa kuyashinda makundi ya waasi, zaidi ya kuwarushia makombora na kutraji kwamba yatawamaliza''. Amesema Vircoulon.
Mtaalamu huyo kutoka ICG amesema mkakati mwafaka ungekuwa kuwafuata waasi hao walikokimbilia na kuendeleza shinikizo la kijeshi dhidi yao, na sio kuwapa wasaa wa kujikusanya tena katika maeneo yaliyo kati ya Ituri na Kivu Kaskazini. Anasema kwa mtazamo wake, MONUSCO na jeshi la Kongo waliridhishwa na operesheni ya mabomu iliyowatimua ADF kutoka ngome zao, na kisha wakawaacha na kuwapa nafasi ya kupumzika katika misitu ya Ituri. ''Sioni uwezekano wowote wa kuwasogelea tena na kufanya nao mazungumzo, huo ni mchakato mgumu hususan kufanywa na watu baada ya kuwashambulia kwa mabomu'', amesema Thierry Vircoulon, na kuongeza kwamba huenda tatizo la ADF likabakia kuwa kama lile la AFDLR kutoka Rwanda na makundi mengine ya waasi katika eneo hilo.
Mwandishi: Maja Brown
Tafsiri: Daniel Gakuba
Mhariri: Hamidou Oummilkheir