DRC yataka walinda amani wa Umoja wa Mataifa kuondoka haraka
21 Septemba 2023Akihutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo jana, Tshisekedi alisema ujumbe huo wa walinda amani wenye askari wapatao 15,000 umeshindwa kukabiliana na uasi wa makundi yenye silaha, kuwalinda raia na hata kurejesha amani nchini humo. Rais huyo wa Kongo amesema ni wakati sasa wa taifa hilo kuchukua hatima yao mikononi.
"Nimeiagiza Serikali kuanza majadiliano na mamlaka za Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha inaharakisha zoezi la kujiondoa kwa MONUSCO kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kubadili muda wa mwisho wa kujiondoa kwa vikosi hivyo kutoka Desemba 2024 hadi Desemba 2023," alisema rais Tshisekedi.
Waliouawa maandamano DRC wazikwa
Kwa miaka kadhaa sasa, suala la kuondoka kwa vikosi vya MONUSCO limekuwa kiini cha mijadala na mivutano hasa kuhusu mustakabali wa taifa hilo la Afrika ya Kati.
Mnamo mwaka 2020, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha mpango wa kujiondoa kwa awamu nchini Kongo.