1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan ataka uwepo utulivu

3 Juni 2013

Huku Uturuki ikiingia siku yake ya nne ya maandamano, Waziri Mkuu Tayyip Erdogan ametoa wito wa kuwepo kwa utulivu, akiwaita waandamanaji kuwa "kundi la wahuni" na waandamanaji nao wakiendelea kukabiliana na polisi.

https://p.dw.com/p/18imv
An anti-government protester gestures during a demonstration in Ankara late June 2, 2013. Tens of thousands of people took to the streets in Turkey's four biggest cities on Sunday and clashed with riot police firing tear gas in the third day of the fiercest anti-government protests in years. Prime Minister Tayyip Erdogan blamed the main secular opposition party for inciting the crowds, whom he called "a few looters", and said the protests were aimed at depriving his ruling AK Party of votes as elections begin next year. REUTERS/Umit Bektas (TURKEY - Tags: POLITICS CIVIL UNREST)
Türkei Proteste Regierung IzmirPicha: Reuters

Akiwa uwanja wa ndege wa Istanbul kuelekea Morocco mapema leo, Erdogan amewataka wananchi wa Uturuki kutokuchokozeka kirahisi na wa maandamano aliyosema yameandalaiwa na "watu wenye siasa kali,"

"Tulieni. Haya yote yatatatuliwa. Waandamanaji wamekuwa wakivunja kingo za barabara na wakivunja maduka ya watu. Je, hiyo ndiyo demokrasia? Wanasema Tayyip Erdogan ni dikteta. Mimi sina la kusema ikiwa wanamuita dikteta mtu aliyejitolea kuitumikia nchi yake." Alisema Erdogan mbele ya waandishi wa habari.

Mjini Istanbul kwenyewe, mapambano yameripotiwa kuendelea kati ya polisi na waandamanaji kwa siku ya nne leo. Shirika la habari la Dogan limesema kuwa polisi walitumia gesi ya machozi dhidi ya waandamanaji waliokusanyika karibu na ofisi za Erdogan asubuhi ya leo. Waandamanaji nao wakajibu kwa kurusha mawe.

Watu kadhaa wakamatwa

Kwa mujibu wa shirika hilo, kiasi cha waandamanaji 500 wamekamatwa usiku wa kuamkia leo, baada ya polisi kuvunja maandamano mengine yaliyohudhuriwa na maelfu ya watu kwenye mji mkuu, Ankara. Kituo cha televisheni cha Fox cha Uturuki kimeripoti kwamba watu wengine 300 wamekamatwa katika mji wa Izmir, ambao ni wa tatu kwa ukubwa nchini humo.

Polisi wakitumia mabomu ya machozi kutawanya waandamanaji.
Polisi wakitumia mabomu ya machozi kutawanya waandamanaji.Picha: picture-alliance/AP Photo

"Katika hali kama hii, polisi kutumia nguvu zisizolingana hakukubaliki. Polisi wanapaswa kuwalinda watu," alisema mwandamanaji mmoja mjini Istanbul, akielezea sababu za kushiriki kwenye maandamano hayo.

Vuguvugu dhidi ya Erdogan

Chanzo cha maandamano ni hasira za wananchi dhidi ya matumizi ya nguvu ya kupita kiasi yaliyofanywa na polisi kwa kundi dogo la wanaharakati wa mazingira. Awali waandamanaji hao walikuwa wakipinga tu mpango wa serikali kujenga kwenye uwanja wa Taksim, katikati ya Istanbul, lakini sasa wameyageuza kuwa vuguvugu la mageuzi dhidi ya serikali ya Erdogan.

Waandamanaji mjini Istanbul.
Waandamanaji mjini Istanbul.Picha: Reuters

Haya yanasemekana kuwa maandamano makubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini Uturuki, tangu chama cha Erdogan, chenye misingi ya Kiislamu, kuingia madarakani, takribani miaka kumi sasa.

Ndani ya kipindi hicho cha muongo mmoja, chama cha AK kimeongeza kura zake kwenye chaguzi tatu mfululizo na kushinda kwenye kura mbili za maoni.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman