Erdogan aweka sharti jipya kwa Sweden kujiunga na NATO
10 Julai 2023Msimamo huo mpya katika juhudi za Sweden kupata uungwaji mkono wa Erdogan umekuja siku moja kabla ya Mkutano wa kilele wa wakuu wa mataifa wanachama wa jumuiya ya NATO katika mji mkuu wa Lithuania, Vilinius, ambapo viongozi wa magharibi wanataka kuonyesha umoja mbele ya vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.
Tamko hilo ambalo Erdogan amelitoa kabla ya kuanza safari ya kuhudhuria mkutano wa kilele wa NATO katika mji mkuu wa Lithuania limeongeza mashaka katika maombi ya Sweden kuwa mwanachama wa 32 wa muungano huo, ambayo Uturuki iliyazuia mwanzoni ikisema Sweden ilikuwa inachukuwa msimamo laini sanakuhusu wanamgambo wa Kikurdi na makundi mengine ambayo Ankara inayachukulia kuwa ni vitisho vya usalama.
Soma pia: Maafisa wa Sweden na Uturuki kukutana mjini Brussels
Hii ndiyo mara ya kwanza kwa Erdogan kuhusisha harakati za nchi yake kujiunga na Umoja wa Ulaya na juhudi za Sweden kuwa mwanachama wa NATO.
"Uturuki imekuwa ikisubiri mlangoni mwa Umoja wa Ulaya kwa zaidi ya miaka 50 sasa, na karibu nchi zote wanachama wa NATO sasa ni wanachama wa Umoja wa Ulaya. Ninatoa wito huu kwa nchi hizi ambazo zimeifanya Uturuki kusubiri kwenye lango la Umoja wa Ulaya kwa zaidi ya miaka 50,” Erdogan alisema.
"Njooni mfungue njia kwa uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya. Unapofungua njia kwa Uturuki, tutafungua njia kwa Sweden kama tulivyoifanyia Finland,” aliongeza.
Sweden bado ina matumaini
Mapema ofisi ya Erdogan ilisema alimuambia rais wa Marekani Joe Biden wakati wa mazungumzo kwa njia ya simu siku ya Jumapili kwamba Uturuki ilitaka ujumbe thabiti na wa wazi wa uungwaji mkono wa malengo yake ya kujiunga na Umoja wa Ulaya kutoka viongozi wa NATO wanaokutana mjini Vilnius.
Erdogan na waziri mkuu wa Sweden Ulf Kristersson walitarajiwa kukutana baadae leo mjini Vilnius.
Uturuki imekuwa ikiwania kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, lakini maombi yake ya uanachama yamekwama kutokana na kile kinachodaiwa kuwa kuporomoka kwa demokrasia pamoja na mizozo na Cyprus ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Mapema Jumatatu, waziri wa mambo ya nje wa Sweden, Tobias Billström, alielezea matumaini kwamba Uturuki itaachana na upinzani wake kwa wanachama wa Sweden, akisema hilo sasa ni suala la lini na siyo iwapo.
Stoltenberg asema Sweden imetimiza masharti ya Uturuki
Alipoulizwa kuhusu kauli za Erdogan, Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, amesema anaunga mkono malengo ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya, lakini amebainisha kuwa hilo halikuwa miongoni mw amasharti yalioorodheshwa katika makubaliano ambayo Sweden, Finland na Uturuki zilisaini katika mkutano wa kilele wa NATO mjini mAdrid mwaka jana.
Soma pia: Erdogan apuuza shinikizo la kumuidhinisha Sweden uanachama wa NATO
Stoltemberg amekariri kuwa Sweden imetimiza masharti hayo na kusema anadhani bado inawezekana kuwa na uamuzi chanya kuhusu uanachama wake wakati wa mkutano wa wiki hii nchini Lithuania.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema analitazama tamko la Erdogan kama hatua chanya, kwamba Uturuki inaweza kufikiria kwamba Sweden inaweza kujiunga na NATO, lakini pia amesisitiza kwamba maombi ya Sweden hayapaswi kuhusishwa na harakati za Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Chanzo: Mashirika