1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erik ten Hag ajilaumu kwa sare dhidi ya Galatasaray

30 Novemba 2023

Mkufunzi wa Manchester United Erik ten Hag amesema anafaa kulaumiwa kwa klabu yake kupoteza uongozi mwingine katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya baada ya kulazimishwa sare ya 3-3 na Galatasaray.

https://p.dw.com/p/4ZbeA
Erik ten Hag | Kocha | Manchester United
Kocha wa Manchester United Erik ten HagPicha: Andrew Yates/Sportimage/Cal Sport Media/picture alliance/Newscom

Mabingwa hao mara tatu wa Ulaya walipoteza uongozi wa mabao mawili mjini Istanbul, huku mlinda lango Andre Onana akifanya makosa ambayo huenda yakaigharimu klabu hiyo nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora.

Manchester United wako mkiani mwa kundi A ikiwa na alama nne baada ya kucheza mechi tano, alama moja tu nyuma ya Copenhagen na Galatasaray.

Mashetani Wekundu hao ni lazima waifunge Bayern Munich mnamo Disemba 12 ili kujiweka katika nafasi ya kufuzu hatua ya 16 bora.

Soma pia: Kina nani watakaonyakua nafasi 10 za mtoano Champions League?

United iliacha uongozi wa mabao mawili kwa moja katika mchezo wa awali dhidi ya Copenhagen na hatimaye kupoteza kwa mabao 4-3, huku Erik ten Hag akielezea masikitiko ya klabu hiyo ya kushindwa kudhibiti mchezo wanapotangulia kufunga.

Kiungo wa Manchester United Bruno Fernandes
Nahodha wa Manchester United Bruno FernandesPicha: picture alliance/empics

"Siku zote mimi ndio wa kulaumiwa kwa timu kupoteza uongozi baada ya kutangulia kufunga mabao. Ninawajibikia hilo, lakini bado naamini tuko kwenye mradi," raia huyo wa Uholanzi ameliambia shirika la habari la michezo la TNT.

"Tupo kwenye mwelekeo sahihi, nafahamu ni wapi tunapotakiwa kwenda na hatua gani tunazopaswa kupiga lakini nina uhakika tutafanikiwa. Iwapo tunataka kusalia kwenye michuano ya ligi ya mabingwa, lazima tushinde mchezo unaofuata."

Mkufunzi huyo ameonyesha imani kuwa, klabu hiyo ya Uingereza hatimaye itapata suluhu ya kuruhusu kufungwa mabao mengi.

Vijana wa Erik ten Hag watasafiri kuelekea ugani St James Park kucheza dhidi ya Newcastle United siku ya Jumamosi katika mechi ya ligi kuu ya Premia.