1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia imemchagua afisa wa TPLF kuwa rais wa mpito Tigray

23 Machi 2023

Serikali ya Ethiopia imemteua afisa mkuu wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray, TPLF kuwa kiongozi wa serikali ya mpito upande wa Tigray baada ya makubaliano ya amani yaliyositisha mapigano yaliyodumu miaka 2

https://p.dw.com/p/4P9UV
Pretoria | Waffenstillstandsabkommen für Äthiopien
Picha: Themba Hadebe/AP/picture alliance

Tangazo hilo limekuja siku moja baada ya bunge la Ethiopia, kukiondoa chama cha TPLF katika orodha ya makundi ya kigaidi, hatua iliyosemekana kupiga jeki makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwezi Novemba mwaka jana, kati ya waasi wa Tigray na serikali ya shirikisho.

Taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed, inasema kiongozi huyo amemteua Getachew Reda kama rais wa serikali ya mpito katika jimbo la Tigray. Mpaka sasa hapajatolewa tamko lolote kutoka katika chama hicho cha TPLF au Reda mwenyewe kuhusiana na uteuzi huo.

TPLF yaondolewa katika orodha ya makundi ya kigaidi Ethiopia

Kuundwa kwa serikali ya mpito na kukiondoa chama cha TPLF katika orodha ya makundi ya kigaidi,  ni miongoni mwa masharti muhimu ya chama hicho katika makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mjini Pretoria Afrika Kusini. Makubaliano hayo yalitaka kuundwa kwa serikali hiyo itakayojumuisha pande zote za kisiasa hadi pale uchaguzi utakapoandaliwa.

TPLF iliyowahi kutawala siasa za Ethiopia liliingizwa rasmi katika orodha ya makundi ya kigaidi mwezi Mei mwaka 2021 miezi sita baada ya mgogoro wa Tigray kuanza.

Getachew ni mshauri wa kiongozi wa  TPLF Debretsion Gebremichael. Aliwahi pia kuwa waziri wa mawasiliano katika serikali ya shirikisho chini ya Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn, aliyeiongoza Ethiopia kuanzia mwaka 2012 hadi 2018.

Makubaliano ya amani yafungua njia ya Maridhiano

Pretoria | Waffenstillstandsabkommen für Äthiopien
Waziri wa Afrika kusini wa uhusiano wa kimataifa na ushirikiano Naledi Pandor, Redwan Hussien Rameto, muakilishi wa serikali ya Ethiopia, rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta,Mjumbe wa Umoja wa Afrika Olusegun Obasanjo, Getachew Reda, muakilishi wa TPLF na naibu rais wa zamani wa Afrika Kusini Phumzile Mlambo-Ngcuka wakipigwa picha ya pamoja baada ya makubalino ya amani kutiwa saini mjini Pretoria. Picha: PHILL MAGAKOE/AFP

Getachew ndiye aliyesaini makubaliano ya amani kwa niaba ya chama hicho pamoja na Redwan Hussein mshauri wa usalama wa taifa katika serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed.

Chini ya makubaliano hayo yaliyoongozwa na Umoja wa Afrika, TPLF ilikubali kuweka chini silaha na kurudishwa tena kwa mamlaka ya shirikisho katika jimbo la Tigray.

Kuanzia wakati huo kumekuwa na mabadiliko chanya katika jimbo la Tigray, kuanzia kurejeshwa huduma muhimu kama mawasiliano, pamoja na huduma za benki  na hata kuruhusu misaada kama chakula, mafuta na dawa kuingizwa katika jimbo hilo lililo na idadi ya watu milioni 6.

Marekani yasema uhalifu wa kivita ulifanywa katika vita vya Tigray nchini Ethiopia

Mapigano yalianza wakati Serikali ya Ethiopia ilipoituhumu TPLF kuanzisha mgogoro kwa kushambulia kambi yake ya jeshi katika jimbo la Tigray, huku TPLF nao wakiituhumu serikali hiyo ya shirikisho kuwa ilikuwa tayari imeshajitayarisha kuishambulia. Mapigano hayo yalisababisha mauaji ya watu takriban laki sita huku wengine wengi wakipoteza makaazi yao. 

Blinken aiomba Ethiopia kuimarisha amani baada ya vita

Vita vya Tigray viliiharibu sifa ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliyewahi kushinda tuzo ya amani ya Nobel huku Marekani ikidai kwamba wanajeshi wa serikali na washirika wake nchi jirani ya Eritrea, walitekeleza uhalifu dhidi ya binaadamu wakati wa vita hivyo. Siku ya Jumatatu ilizituhumu pande zote katika mgogoro huo kutekeleza uhalifu wa kivita bila ya kuwataja moja kwa moja wapiganaji wa TPLF.

Chanzo: afp/ reuters