1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

George Floyd aagwa na mamia Minneapolis

5 Juni 2020

Watu mashuhuri, wanamuziki na viongozi wa kisiasa nchini Marekani walikusanyika mbele ya jeneza la George Floyd, katika ibada ya misa iliyojaa mihemko kumuaga Floyd ambaye kifo chake kimesababisha maandamano kote duniani

https://p.dw.com/p/3dIvT
USA Minneapolis Gedenkfeier für George Floyd
Picha: Getty Images/AFP/K. Yucel

Ibada hiyo ya kumuaga George Floyd ambayo ni ya kwanza kufanyika katika miji mitatu tofauti ndani ya siku sita, iliyoanzia mjini Minneapolis, katika eneo takatifu kwenye chuo kikuu cha North Central huku jaji mmoja katika eneo karibu na hilo akitoa dhamana ya dola 750,000 kwa kila mmoja ya maafisa watatu wa polisi walioshitakiwa kwa kushiriki katika mauaji ya George Floyd.

''Kilichomtokea George Floyd ndio changamoto wanayopitia watu weusi tangu miaka 401 iliyopita, na hii ndio sababu ya kutufanya sisi tusiwe kile tunachotaka kuwa mmekuwa mkiweka goti lenu kwenye shingo zetu, ni wakati wa kusimama na kutumia sauti ya Floyd, kusema ondoeni goti lenu kwenye shingo zetu'' alisema Mchungaji Al Sharpton aliyeongoza bada hiyo ya kukumbuka maisha ya Floyd.

Ameongeza kuwa kile kinachoshuhudiwa kwa sasa kitakuwa vuguguvu linalonuiwa kubadilisha mfumo wa haki nchini Marekani.

Wale waliokusanyika katika ibada hiyo mjini Minneapolis walinyamaza kwa dakika 8 sekunde 46 ambao ni muda unaodaiwa Floyd alikuwa amewekwa chini na kuwekewa goti na polisi hadi mauti yalipomfika. Waombolezaji waliovalia barakoa zilizoandikwa "sasa naweza kupumua" walibubujikwa na machozi huku wengine wakiomba dua kwa sauti.

Miongoni mwa waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na mchungaji Jesse Jackson, seneta Amy Klobuchar na wanachama kadhaa wa bunge la congress akiwemo wabunge  wa chama cha democratic Ilhan Omar, Sheila Jackson Lee na Ayanna Pressley. Wengine ni wasanii mashuhuri nchini Marekani akiwemo T.I., Ludacris, Tyrese Gibson, Kevin Hart, Tiffany Haddish na Marsai Martin.

Floyd, aliyekuwa na miaka 46 aliuwawa Mei 25 baada polisi mweupe Derek Chauvin, kumuwekea goti lake shingoni huku akiwa amelala chini na mikono yake kufungwa pingu. Chauvin ameshitakiwa kwa mauaji na yeye pamoja na maafisa wengine watatu huenda wakakabiliwa na hukumu ya hadi miaka 40 jela.

Maadamano ya kupinga ukatili wa polisi bado yaendelea Marekani

Österreich Wien Demonstration gegen Rassismus nach Tod von George Floyd
Picha: Reuters/L. Foeger

Huku hayo yakiarifiwa watu katika miji tofauti ikiwemo Paris, London, Sydney na Rio de jeneiro wameendelea kuandamana dhidi yaukatili wa polisi, ubaguzi wa rangi, na ukosefu wa usawa.

Mjini Ney York pia maandamano yaliendelea waandamanaji wakibeba mabango yalioandikwa Floyd hauko peke yako. Kakaake Floyd Terrence Floyd alisema kila kinachoendelea kinaonesha namna flody alivyokuwa mtu wa watu na kuendelea kusisitiza haki kwa Floyd.

Wakati huo huo muungano wa ukombozi wa raia na makundi mengine yakiwemo kundi la Black Lives Matter na baadhi ya waandamanaji wamefungua keshi dhidi ya serikali ya Rais Donald Trump wakidai kuwa maafisa wa serikali hiyo wamekiuka haki  ya raia ya kuandamana.

Waandamanaji waliondolewa karibu na eneo moja la wazi lililo karibu na ikulu ya Marekani na polisi waliowarushia mabomu ya kutoa machozi na maji ya pilipili. Badaa ya waandamanji kutawanywa rais Trump alielekea katika kanisa moja lililoko karibu kupiga picha . Kundi hilo limelielezea tukio hilo kama la kupanga na la kuwadhalilisha na kuwakasirisha zaidi waandamanaji.

Chanzo: afp,ap,reuters