Hali bado ni mbaya Mashariki ya Kati
16 Oktoba 2015Wanadiplomasia wamesema mkutano huo wa dharura umeitishwa na Jordan ambayo ni mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kufuatia mkutano wa mabalozi wa mataifa ya Kiarabu uliofanyika jana, kuelezea wasiwasi wao kuhusu kuongezeka kwa ghasia hizo mjini Jerusalem, huku kukiwa na hofu ya kuzuka kwa vuguvugu la mapambano na Wapalestina - Intifada ya tatu.
Mkutano huo utafanyika wakati ambapo Wapalestina kadhaa leo wamerusha mabomu kwenye eneo takatifu linalokaliwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi, huku wengine wakitoa wito wa kufanyika mapinduzi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amerejelea wito wake wa kuwepo utulivu kutokana na wiki kadhaa za ghasia ambazo zimesababisha vifo vya kiasi ya Wapalestina 30 na Waisraeli saba.
Mjumbe wa Palestina, Riyad Mansour, amewaambia waandishi wa habari kwamba hali ni tete na amelitaka baraza hilo kuonyesha wajibu wake kwa kuchukua hatua za kukabiliana na ghasia hizo.
Marekani yaunga mkono taarifa kuhusu matumizi ya nguvu
Marekani imeungana na mataifa yanaiyokosoa Israel kutokana na nguvu za kijeshi zinazotumika. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, John Kirby amesema wameona taarifa kuhusu kile ambacho wengi wanaweza kusema ni matumizi ya nguvu yaliyopindukia.
Lakini Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema Israel inatumia nguvu halali katika kukabiliana na mashambulizi ya Wapalestina.
''Israel inatumia aina ya nguvu sawa na ambayo serikali yoyote ile, manispaa na vikosi vya polisi zingetumia kama walikuwa na watu wanaobeba visu na mashoka na kujaribu kuwaua watu kwenye mitaa yao,'' alisema Netanyahu.
Hata hiyo, Netanyahu ameendelea kusisitiza kuhusu nia yake ya kukutana na kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas, huku akimtuhumu kwa kuchochea na kuhamasisha ghasia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, pia amemuonya Abbas kutochochea ghasia. Kerry ambaye anapanga kuzuru katika ukanda huo, amesema Rais Abbas anatakiwa kukemea ghasia hizo.
Israel yapeleka majeshi ya usalama Jerusalem
Hayo yanajiri wakati ambapo Israel imepeleka majeshi yake ya usalama mjini Jerusalem, wakati Wayahudi wenyewe wakijihami kwa silaha mbalimbali kuanzia bunduki hadi mifagio. Wanajeshi wapatao 300 wanalisaidia jeshi la polisi ambalo limeelemewa na kuenea kwa ghasia hizo.
Ama kwa upande mwingine, Wapalestina wameitisha maandamano yenye lengo la kuelezea hasira yao. Maandamano hayo yanatarajiwa kufanyika leo kwenye eneo linalokaliwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, baada ya Swala ya Ijumaa.
Na katika kuonyesha mshikamano na kuwaunga mkono Wapalestina, mashirika ya Wapalestina leo yameandaa maandamano mengine mjini Berlin. Hata hivyo, Baraza Kuu la Wayahudi nchini Ujerumani, limetoa wito wa maandamano hayo kupigwa marufuku.
Aidha, Polisi ya Israel imetangaza kutokana na sababu za kiusalama, ni wanaume wenye zaidi ya umri wa miaka 40 pekee ndiyo wataruhusiwa kuingia kwenye Hekalu la Mlima Jerusalem, eneo takatifu kwa Waislamu.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman