1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres ahimiza uratibu wa kimataifa katika vita vya COVID

17 Desemba 2021

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema itakuwa vigumu kulidhibiti janga la COVID-19 iwapo hakutakuwa na uratibu wa pamoja kimataifa katika vita dhidi ya janga hilo.

https://p.dw.com/p/44P3r
Antonio Guterres  I UN
Picha: John Minchillo/POOL/AP/picture alliance

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anatoa onyo hilo wakati Ulaya kupitia taasisi ya usimamizi wa dawa, EMA ikiidhinisha matumizi ya dawa mpya ya COVID-19, kutokana na kitisho kinachotokana na ongezeko la maambukizi ya aina mpya ya kirusi cha corona, Omicron

Guterres ametoa matamshi hayo jana Alhamisi katika ujumbe wake wa mwisho wa mwaka. Amesema chanjo pekee hazijitoshelezi katika vita dhidi ya janga hilo huku akiendelea kusisitizia kitisho kinachoweza kusababishwa na kukosekana kwa usawa wa chanjo ulimwenguni.

Amesema, kukosekana huko kwa usawa kunatoa mwanya kwa virusi vya corona kusambaa kwa kasi na kuathiri afya ya watu na mataifa kote ulimwenguni.

"COVID-19 haitakwisha. Inadhihirika kwamba chanjo pekee haziwezi kumaliza janga hili. Chanjo zinazuia kulazwa hospitalini na vifo kwa wengi wanaochanjwa, lakini pia kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi. Lakini maambukizi hayaonyeshi dalili ya kupungua. Na hii inachochewa na ukosefu wa usawa wa chanjo, kusitasita na kuridhika." alisema Guterres.

Kutokana na hilo, Guterres ameyaomba mataifa kukubaliana namna ya pamoja ya kupambana na COVID-19 na kusisitizia umuhimu mabadiliko katika mfumo wa fedha wa kimataifa.

Niederlande | EMA Hauptquartier in Amsterdam
Taasisi ya usimamizi wa dawa barani Ulaya, EMA imeidhinisha aina mpya za dawa ili kupambana na ongezeko la maambukizi ya COVID-19Picha: Peter Dejong/AP Photo/picture alliance

Huku Guterres akiangazia hilo, barani Ulaya, Taasisi ya usimamizi wa dawa, EMA imeidhinisha jana matumizi ya aina mbili za dawa za kutibu maradhi ya COVID-19 pamoja na matumizi ya dharura ya aina ya tatu ya dawa.

Soma Zaidi: Viongozi wa Kiafrika walihutubia Baraza la Umoja wa Mataifa

Marekani sasa yahimiza raia wake kutumia aina nyingine ya chanjo, badala ya J&J.

Dawa zilizothibitishwa ni Sotrovimab inayotengenezwa kwa pamoja na kampuni ya dawa ya Uingereza ya GlaxoSmithKline na Vir Biotechnology ya Marekani. Kulingana na EMA, Dawa hiyo inapunguza hatari ya wagonjwa walio na dalili hatarishi kulazwa hospitalini ama kufariki. Aina ya tatu ya dawa iliyodhinishwa kutumika kwa dharura ni Xeduvy.

EMA pia imeidhinisha matumizi ya dharura ya vidonge vya COVID-19 vya Pfizer na kusema dawa hiyo inaweza kutumika kuwatibu watu wazima walioambukizwa COVID-19 na wasiohitaji Oksijeni, lakini wanaweza kupata dalili mbaya zaidi.

Kinachosubiriwa sasa ni tume ya Ulaya yenye mamlaka ya mwisho ya kuidhinisha matumizi ya dawa hizo.

Nchini Marekani, idara za kupambana na kudhibiti magonjwa hapo jana ziliwataka raia nchini humo kuchagua kupata chanjo za aina nyingine mbili zilizoidhinishwa nchini humo, mbali na Johnson&Johnson kutokana na visa vya kuganda kwa damu. Kamati ya ushauri ya CDC ilikubaliana kwa umoja kuidhinisha chanjo za Moderna na Pfizer/Biontech, badala ya J&J.

Wataalamu wa CDC wamesema hatari ya kuganda damu iko juu ikilinganishwa na ilivyodhaniwa awali kwa wanaume na wanawake, na tayari takriban watu tisa wamefariki kutokana na tatizo hilo.

Soma Zaidi: AstraZeneca: Madaktari Wajerumani wagundua chanzo cha mvilio wa damu

Mashirika: DW/APTN