Guterres atolea wito jamii ya kimataifa kuisaidia Haiti
7 Julai 2023Guterres amesema kwamba makadirio ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwamba Haiti inahitaji polisi wa kukabiliana na magenge hadi 2000 sio uzushi. Kauli hii inajiri baada ya mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini humo Maria Isabel Salvador, kusema takriban washukiwa 264 wa magenge ya uhalifu wameuawa na walinzi tangu Aprili.
Soma pia: Guterres: jeshi la kimataifa linapaswa kupelekwa Haiti
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi zinazoweza kuchangia katika kile alichokitaja kama "kuchukua hatua " na kupeleka jeshi la kimataifa kusaidia Polisi wa Kitaifa wa Haiti kukabiliana na magenge.
Gutteres amesema "Watu wa Haiti wanaishi katika hali mbaya. Hali ya kibinadamu ni ya kutisha sana. Magenge ya kikatili yanawahangaisha watu wa Haiti. Port-au-Prince imezingirwa na makundi yenye silaha ambayo yanafunga barabara, yamechukua udhibiti wa upatikanaji wa chakula, na huduma za afya na kudhoofisha msaada wa kibinadamu."
Aliendelea kusema "Magenge hayo yanatumia utekaji nyara na unyanyasaji wa kingono kama silaha kutisha jamii nzima. Ninatoa wito kwa wanachama wa Baraza la Usalama na kwa nchi zote zinazoweza kuchangia kuchukua hatua sasa."
Soma pia: Mtuhumiwa akiri kupanga mauaji ya rais wa Haiti
Haiti imekuwa ikiomba usaidizi tangu mwishoni mwa Oktoba, na Guterres amekuwa akitafuta nchi itakayoongoza kupelekwa kwa jeshi. Marekani na Canada ambao wangeweza kuongoza wamejiondoa.
Jukumu la Umoja wa Mataifa Haiti
Akizungumza katika mkutano na Baraza la Usalama Waziri wa Mambo ya Nje wa Haiti Jean Victor Geneus amesema ni jukumu la Umoja wa Mataifa kulisaidia taifa hilo.
"Umoja wa Mataifa kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa una wajibu wa kimaadili wa kuizuia Haiti kudidimia. Hatua ya Baraza hilo ni madhubuti katika kurejesha matumaini nchini Haiti na kuwawezesha wananchi wa Haiti hasa wale wanaoteseka na walio wengi, kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora. " alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Haiti Jean Victor Geneus.
Soma pia: Hali ni ya kukata tamaa Haiti, UN yaambiwa
Katika kikao cha baraza hilo wajumbe wengi waliunga mkono wito wa katibu mkuu wa kupekwa kwa jeshi la kimataifa lakini hapakuwa na waliojitolea. Jamaica na Bahamas tayari wameonyesha nia yao ya kuchangia katika kikosi cha kimataifa huku Rais wa Guyana Irfaan Ali akisema Rwanda na Kenya pia zimeonyesha nia ya kuchangia.
//AFP, Ap