Guterres: Kuna hatari ya kutanuka mzozo wa Gaza
1 Novemba 2023Guterres amerejelea msimamo wake wa kulaani shambulio la Hamas la Oktoba 7 na kuamuru kuachiwa huru mateka wote, lakini akaalani pia mauaji ya raia huko Gaza na kusisitiza kuwa amesikitishwa na ripoti iliyobainisha kwamba theluthi mbili ya waliouawa huko Gaza ni wanawake na watoto. Hadi sasa, wizara ya afya imesema watu 8,525 wameuawa Gaza huku 3,500, miongoni mwa hao ni watoto.
Ama katika uwanja wa mapambano , jeshi la ulinzi la Israel IDF limeendeleza usiku wa kuamkia leo, mashambulizi yake katika maeneo mbalimbali ya Gaza na limethibitisha kuwa limefanya shambulio kwenye kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa ukanda huo.
Msemaji wa jeshi la Israel Luteni Kanali Richard Hecht ameliambia shirika la utangazaji la Marekani CNN kwamba walimlenga kamanda mkuu wa Hamas aliyekuwa katika eneo hilo. Israel ambayo imekuwa ikifanya operesheni kadhaa za ardhini, imesema pia kuwa wanajeshi wake wawili wote wakiwa na umri wa miaka 20, wameuawa jana Jumanne huko Gaza huku wengine wawili wakijeruhiwa.
Soma pia: Israel yapambana vikali na Hamas ndani ya Gaza
Wizara ya Afya inayodhibitiwa na kundi la Hamas imesema shambulio hilo kwenye kambi ya wakimbizi limesababisha vifo vya watu 50 na kuwajeruhi wengine karibu 150.
NATO na EU zaelezea pia wasiwasi wao
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami NATO, Jens Stoltenberg akihutubia mkutano wa Baraza la Nordic, amelaani mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel na kusema jibu la Israel lazima liheshimu sheria za kimataifa huku akionya kuwa mzozo huo haupaswi kuwa mzozo mkubwa wa kikanda.
Kwa upande wake Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema kuna haja kuanzisha upya na kwa haraka mchakato wa amani huku akitaja wasiwasi mkubwa kufuatia mashambulizi ya walowezi wa kiyahudi dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel.
Nchini Marekani waandamanaji walikatiza na kuvuruga kikao cha Bunge wakati Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken na Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin walipokuwa wakizungumza na kuitaka kamati ya maseneta kuidhinisha ufadhili wa mabilioni ya dola katika sekta ya usalama inayojumuisha msaada kwa Israel na Ukraine.
Soma pia: Gaza kutumbukia janga la kiafya - WHO
Waandamanaji hao waliokadiriwa kufikia 24 ambao baadaye walitawanywa na polisi, walifanikiwa kuingia ndani ya Bunge hilo la Marekani na walikuwa wamepaka rangi nyekundu mikono yao kama ishara ya damu na kuiweka juu huku wakipaza sauti zao na kusema: " Sitisheni mapigano sasa, Walindeni watoto wa Gaza, Sitisheni ufadhili wa mauaji ya kimbari". Marekani ndiyo mshirika mkuu wa kiusalama wa Israel.