Gutteres atoa wito wa kusitishwa mapigano Tigray, Ethiopia
6 Novemba 2020Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres, Ijumaa ametowa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano hayo, akisisitiza kwamba hali ya utulivu nchini Ethiopia ni muhimu kwa eneo zima la Pembe ya Afrika.
"Utulivu wa Ethiopia ni muhimu kwa Pembe nzima Afrika. Natowa wito wa kutatuliwa huu mzozo kwa njia ya amani," ameandika Gutteres katika ujumbe kwake wa Twitter.
Hadi Ijumaa asubuhi, sauti za mizinga na risasi zilikuwa zikisikika kutoka mji wa Aburafi, ambao upo mpakani mwa majimbo ya Tigray na Amhara. Ndege mbili za kijeshi za Ethiopia zilionekana zikiruka kwenye anga la mji mkuu wa Tigray, Mekelle, jana jioni, kwa mujibu wa vyanzo vya kibalozi vilivyozungumza na shirika la habari la Reuters.
Soma zaidi: Ethiopia yashinikizwa kusimamisha kampeni ya kijeshi Tigray
Hiyo ni baada ya hapo jana mamlaka ya anga kuamua kulifunga anga la mkoa huo kwa ndege za kiraia za ndani na za kimataifa. Televisheni ya jimbo la Tigray imesema kuwa ndege hizo za kijeshi zilishambulia maeneo mawili kwenye mji mkuu Mekelle, lakini hilo halijathibitishwa na upande wa serikali.
Jeshi la Ethiopia limelazimishwa kwenda vitani
Naibu Mkuu wa Jeshi Birhanu Jula, amesema anasikitika sana kwamba jeshi lake limelazimishwa kuingia kwenye vita visivyotegemewa na visivyo na maana na mkoa wa Tigray, ambao inafahamika kwamba umejizatiti muda mrefu kijeshi.
"Nchi yetu imeingia kwenye vita ambavyo haikuvitaka. Vita hivi ni vita vya aibu. Havina msing wowote. Watu wa Tigray na vijana wake na vikosi vyake vya usalama hawapaswi kufa kwa vita hivi visivyo maana. Ethiopia ni nchi yao,” amesema Birhanu Jula Gelalcha Naibu Mkuu wa Jeshi la Ethiopia.
Hata hivyo, naibu mkuu huyo wa jeshi alisema kwamba vikosi vya kijeshi vinaendelea kupelekwa kwenye mkoa huo kutoka maeneo mengine ya nchi, akisema kuwa mapigano hayo yameanzia na yatamalizia huko huko Tigray, akiondosha uwezekano wa vita kusambaa nchi nzima.
Alkhamis, serikali ya Ethiopia ilituma wanajeshi wake wakiwa na silaha kamili za kivita na tayari kwa mapambano kwenye mkoa huo wa kaskazini licha ya wito wa jumuiya ya kimataifa kutaka mzozo baina ya serikali kuu na vikosi vya chama cha Tigray's Liberation Front, TPLF, kumalizwa kwa mazungumzo.
TPLF hawakubaliani na mfumo wa kisiasa wa Ahmed
Watigirinya na chama chao cha TPLF walikuwa ndio kundi kubwa kwenye muungano wa vyama vilivyoongoza serikali ya Ethiopia kwa miongo kadhaa, hadi alipoingia madarakani Abiy Ahmed ambaye anatokea kabila la Oromo, miaka miwili iliyopita.
Abiy, ambaye amekuwa akijaribu kuubadilisha moja ya mifumo mikongwe ya kiuchumi na kisiasa barani Afrika, aliugeuza muungano wa vyama vinavyotawala na kuwa chama kimoja cha kisiasa, lakini TPLF ikakataa kujiunga nao.
Mataifa jirani na Ethiopia yanahofia kwamba mzozo huo unaweza kupelekea vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tayari serikali ya jimbo la Tigray inayoongozwa na Rais Debretsion Gebremichael imesema kwamba ina nguvu na vifaa vya kutosha vya kijeshi kukabiliana na kile ilichosema ni uvamizi kutoka nje.