Hakuna manusura wengine wa ajali ya treni India
3 Juni 2023Mamia ya watu wamejeruhiwa kwenye ajali hiyo inayotajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea bndani ya miongo kadhaa.
Treni hizo ni Coromandel Express iliyokuwa ikisafiri kutoka Howrah, jimbo la Bengali magharibi kuelekea Chena, jimboni Tamil Nadu, na Howrah Superfast Express iliyokuwa ikisafiri kutoka Bengaluru huko Karnataka kuelekea Howrah.
Ajali hiyo iliyozua mtafaruku ilitokea usiku wa Ijumaa umbali wa kilometa 220 kusini magharibi mwa mji wa Kolkata, na kuwalazimu waokoaji kupanda juu ya mabehewa ya treni yaliyoharibiwa na ajali wakivunja milango na madirisha ili kuwaokoa watu waliokuwa ndani.
Idadi ya vifo iliongezeka usiku kucha. Miili ya watu waliofariki dunia iliyofunikwa mashuka meupe ililazwa chini karibu na njia ya reli wakati wenyeji wa eneo ilikotokea ajali na waokoaji walipokuwa wakifanya juhudi kuwasaidia walionusurika.
Wanajeshi na helikopta za jeshi la anga waliunganisha juhudi hizo. Mkurugenzi wa kitengo cha dharura na zimamoto wa jimbo la Odisha, Sudhanshu Sarangi, amesema kufikia majira ya saa nne usiku, walifanikiwa kuwaokoa watu walionusurika na baada ya hapo shughuli iliyofuata ilikuwa ya kuitoa miili ya watu waliokufa kwenye ajali hiyo.
Juhudi za uokoaji usiku kucha
Takribani miili 280 ilipatikana Ijumaa usiku hadi Jumamosi asubuhi. Idadi ya majeruhi inatajwa kufikia watu 900 wakati uchunguzi wa chanzo hasa cha ajali hiyo ukiendelea. Kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa India P.K Jena, kati ya majeruhi hao, waliojeruhiwa vibaya ni 200 na wengine 200 waliruhusiwa kutoka hospitali baada ya kupatiwa matibabu. Raia wengi walijitokeza kutoa damu ili kuyanusuru maisha ya majeruhi.
Hata hivyo, Jena amesema wakati shughuli za uokoaji zikielekea ukingoni, moja ya changamoto kubwa hivi sasa ni kuitambua miili ya waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo. Ameeleza kwamba, ndugu wa marehemu watapatiwa miili ya ndugu zao pale watakapofanikiwa kuthibitisha kwa Ushahidi uhusiano wao na baada ya miili kufanyiwa uchunguzi. Amesema, huenda vipimo vya vinasaba, DNA vikatumika ili kufanya utambuzi.
Mordi awasili eneo la tukio
Waziri mkuu Narendra Modi aliwasili katika eneo ilikotokea ajali hiyo huko Balasore Jumamosi na kuzungumza na waokoaji pamoja na kukagua uharibifu uliotokea. Alifika pia hospitali kuwajulia hali majeruhi.
Msemaji wa wizara ya reli, Amitabh Sharma amesema mamlaka za reli zitaanza kuondoka mabaki ya treni zilizohusika kwenye kisa hicho ili kufanya matengenezo ya reli na kuruhusu kuendelea kwa safari za treni.
Awali, shughuli za uokoaji zilikwenda taratibu kutokana na treni mbili kuminyana. Maafisa wanasema, waokoaji 1200 walifanya kazi na magari ya kubebea wagonjwa 115, mabasi 50 na vituo 45 vya afya vinavyohamishika usiku kucha. Jumamosi imetangazwa rasmi kuwa siku ya maombolezo kwenye jimbo la Odisha.
Licha ya juhudi za serikali za kuimarisha usalama wa reli, ajali nyingi za treni zimekuwa zikitokea kila mwaka katika taifa hilo lenye mtandao mkubwa Zaidi wa reli duniani ulio chini ya usimamizi wa mamlaka moja.
Soma zaidi:Ajali ya treni yaua karibu watu 100 India
Mwezi Agosti 1995, treni mbili ziligongana karibu na New Delhi na kusababisha vifo vya watu 358 katika moja kati ya ajali mbaya zaidi ya treni kuwahi kutokea India.
Mwaka 2016, treni ya abiria iliteleza na kuacha njia yake katikati ya miji ya Indore na Patna ambao watu 146 walifariki dunia. Makosa ya kibinadamu na vifaa vya kutolea ishara vilivyopitwa na wakati ndivyo vinavyolaumiwa kusababisha ajali nyingi kati ya hizo.