1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfrika Kusini

Hatima ya kisiasa wa Rais Ramaphosa iko matatani

Bryson Bichwa2 Desemba 2022

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa anakabiliwa na tishio la kuondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa na Imani naye kutokana na kashfa ya kuwahonga wezi.

https://p.dw.com/p/4KOBy
UK, London | Cyril Ramaphosa Präsident von Südafrika
Picha: Wiktor Szymanowicz/AA/picture alliance

Taarifa hizo za Rais Ramaphosa kufanya mashauriano na watu wake wa karibu, zilianza kuzagaa jana Alhamis baada ya ripoti kutoka kwa jopo la wataalamu wa sheria kudai kwamba rais huyo alificha dola milioni nne pesa taslimu katika shamba lake mwaka 2020.

Alipoulizwa nini hatma ya Rais Ramaphosa Msemaji wa Ikulu Vincent Magwenya alisema mashaurino hayo hayahusiani na chaguo gani linafaa zaidi kwa Rais, bali kinachojadiliwa ni hatua gani ya kuchukua itakayokuwa na manufaa kwa nchi.

Tayari shutuma hizo zinazomkabili rais zimekigawa chama chake na baadhi ya wakongwe wa ANC wamesema hawafurahishwi na mwenendo wa chama hicho kufuatia kuandamwa na madai ya wizi na rushwa kama anavyoeleza Michael Djovu, mpigania uhuru wa watu weusi nchini humu na mwanachama wa ANC.

Uamzi wa chama cha ANC

Kamati kuu ya chama tawala ANC inakutana kujadili kashfa hiyo wiki mbili kabla ya mkutano mkuu wa 55 wa chama tawala kufanyika, ambapo unatarajiwa kuwachagua wajumbe 80 wa halmashauri kuu ya taifa ya chama hicho na viongozi 16 wa juu zaidi akiwemo Rais.

Katika ripoti ya jopo ambalo lilipata ushahidi wa awali inasema kwamba, Rais Ramaphosa huenda alikiuka kiapo chake cha urais baada ya kukutwa dola milioni 4 pesa taslimu shambani kwake huko Limpopo madai ambayo anakanusha na kusema alizipata kutokana na mapato ya nyati waliouzwa kwa raia wa Sudan Mustafa Mohamed Ibrahim Hazim mwaka 2019.