Hatimaye Miguna Miguna arejea nchini Kenya
20 Oktoba 2022Miguna Miguna alipokewa kwa shangwe katika uwanja wa ndege wa kimataifa JKIA jijini Nairobi huku familia yake na wakaazi katika jimbo la Kisumu alikozaliwa wakimsubiri kwa hamu na ghamu.
Miaka minne iliyopita, Miguna Miguna alifurushwa nchini Kenya huku serikali ikiweka kikwazo cha kutoruhusiwa nchini kwa kauli kwamba alikinai uraia wake, hatua hii ikiibua hisia mbali mbali za kisiasa.
Miguna Miguna azuiliwa tena kurudi kwao Kenya
Katika mazungumzo yake ya kwanza na vyombo vya habari katika uwanja wa ndege, ametoa shukrani za dhati kwa rais William Samoei Ruto kwa hatua yake kuondoa kikwazo dhidi yake na pia kwa Wakenya aliowataja kusimama na yeye na kuzingatia sheria.
"Natoa shukrani zangu za dhati kwa wakenya waliokumbatia sheria katika kushinikiza haki zangu," amesema Miguna Miguna.
Mahakama Kenya yawapiga faini waziri, mkuu wa polisi
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Miguna ameandika kauli zinazotafsiriwa kuashiria mipango yake ya Kisiasa hasaa katika siasa za eneo la Nyanza kando na kitaifa huku ikikumbukwa kuwa aliwahi kuwa mshauri wa kinara wa muungano wa Azimio Raila Odinga na hata kushiriki katika kuapishwa kwa Raila Odinga kama rais wa wananchi mnamo Januari 2018 kabla ya uhusiano kati ya wawili hao kuingia doa.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Arnold Osano amesema ujio wa Miguna huenda ukaibua misimamo tofauti ya kisiasa miongoni mwa wakaazi wa eneo la Nyanza, ng'ome ya Odinga.
Miguna Miguna asema alileweshwa kabla ya kupelekwa Dubai
"Kinachosubiriwa ni hatua yake ya kisiasa," amesema Osano.
Kwa wanafamilia wa Miguna, wakiongozwa na ndugu yake Erick Ondiek Miguna anasema, ni furaha kubwa kwa ndugu yao kukubaliwa kurejea nchini akisisitiza kuwa, licha ya madhila dhidi yake, wameamua kusahau na kuganga yajayo huku wakaazi wa Kisumu wakiwa na kauli mbali mbali za ujio wa Miguna ambaye wengi wamemtambua kama mtoto wao.
"Kila mmoja amefurahia maana ni mengi yaliyofanyika bila yeye kuwepo alisema, atapenda kushiriki ukumbusho wa matanga yaliyotokea," amesema Ondiek.
Baada ya kutua uwanja wa ndege, Miguna alielekea moja kwa moja hadi bustani ya Uhuru ambako maadhimisho ya siku ya Mashujaa yanaendelea.