Hezbollah yavurumisha makombora na kuua askari 4 wa Israel
14 Oktoba 2024Jeshi la Israel limesema limedungua makombora kadhaa yaliyovurumishwa kutoka Lebanon na kulilenga eneo la katikati mwa Israel. Shambulio la Hezbollah la siku ya Jumapili katika kambi ya kaskazini mwa Israel liliua wanajeshi wanne wa Israel na kuwajeruhi wengine wapatao 67.
Aidha, Israel inaendelea kupambana kwa wakati mmoja na wanamgambo wa Hamas huko Gaza na wale wa kundi la Hezbollah nchini Lebanon huku vifo vikiripotiwa kila upande.
Tukielekea katika Ukanda wa Gaza, watu 24 wameuawa na makumi wengine wakiwemo watoto wamejeruhiwa kufuatia shambulizi la anga la Israel huko Nuseirat na katika moja ya jengo la hospitali ya Al-Aqsa katika mji wa Deir al-Balah, lililokuwa likiwahifadhi Wapalestina waliokimbia makazi yao.
Wakati vita vikiendelea na hali ya kibinaadamu ikizidi kuwa mbaya, Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris ametoa wito wa kuwasilisha msaada zaidi kaskazini mwa Gaza huku akiitaka Israel kuchukua hatua za ziada ili kuwezesha mtiririko huo wa misaada ya kiutu.
Harris ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa X kwamba Umoja wa Mataifa unaripoti kwamba hakuna chakula kilichoingia kaskazini mwa Gaza kwa karibu wiki mbili sasa huku akisisitiza kuwa sheria ya kimataifa ya kibinadamu ni lazima iheshimiwe kwa raia kulindwa, kupata chakula, maji na dawa.
Soma pia: Papa Francis atoa wito wa kusitisha mapigano huko Mashariki ya Kati
Umoja wa Mataifa umezindua awamu ya pili ya chanjo ya polio kwa watoto huko Gaza. Takriban watoto 590,000 walio chini ya umri wa miaka kumi watapewa chanjo hiyo. Israel na waandaaji wamekubaliana kusitisha mapigano katika eneo mahususi kwa ajili ya sababu za kibinadamu.
Viongozi EU na UK kukutana kuujadili mzozo huu
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Lammy atakutana hivi leo nchini Luxembourg na mawaziri wenzake kutoka Umoja wa Ulaya ili kuujadili kwa kina mzozo huo wa Mashariki ya Kati ambao unatishia kutanuka zaidi.
Tukielekea nchini Lebanon, Israel imeendelea pia kukabiliwa na lawama kutokana na kushambulia kituo cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL . Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema vitendo havikubaliki kabisa.
"Nchi wanachama 27 wa Umoja wa UIaya zimeafikiana kuitaka Israel iache kabisa kuishambulia UNIFIL. Wanachama wengi wa Ulaya wanashiriki katika ujumbe huu. Kazi yao ni muhimu sana. Haikubaliki kabisa kushambulia wanajeshi wa Umoja wa Mataifa."
Israel imevitaka vikosi hivyo kuondolewa eneo la kusini mwa Lebanon ambako mapambano yamekuwa makali dhidi ya Hezbollah.
Vyanzo: (DPAE, AP, AFP)