1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Jeshi la Mali liliwaua watu 300 mwezi Machi

5 Aprili 2022

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema wanajeshi wa Mali na washirika wake wa kigeni waliwaua takriban raia 300, miongoni mwao wanamgambo katika mji wa Moura mwishoni mwa Machi 2022.

https://p.dw.com/p/49TRi
Mali Oberst Assimi Goita, Anführer der malischen Militärjunta
Picha: Annie Risemberg/AFP/Getty Images

Miongoni mwa waliouwawa ni wanamgambo wenye itikadi kali za dini ya Kiislamu.

Kulingana na Human Rights Watch, waliouawa walikamatwa kufuatia operesheni ya kijeshi iliyoanza Machi 27.

Tukio hilo limetajwa kuwa baya zaidi katika machafuko ya Mali ambayo yamedumu kwa muongo mmoja sasa.

Wachunguzi wa shirika hilo la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch walifichua kwamba katika siku za mwisho za Machi, wanajeshi wa Mali na washirika wao wa kigeni, ambao duru nyingi ziliwatambua kama waliotoka Urusi, waliwaua mamia ya watu waliokamatwa katika makundi madogomdogo mjini Moura.

Taarifa ya wizara ya Ulinzi ya Mali iliyotolewa Aprili 1, ilisema jeshi liliwaua watu waliotajwa kuwa magaidi 203 na kuwakamata wengine 51.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa hatua hiyo ilijiri kufuatia  ripoti zilizosambazwa kwa kiasi kikubwa kwenye mitandao ya kijamii   kuhusu mauaji ya raia wengi katika eneo la Maoura. 

Shuhuda mmoja aliyeona kwa macho yake jinsi watu kadhaa walivyouawa kabla ya yeye kuachiliwa Machi 31, amesema aliishi katika woga mwingi kila sekunde akihofia naye atauawa hivyo.
Shuhuda mmoja aliyeona kwa macho yake jinsi watu kadhaa walivyouawa kabla ya yeye kuachiliwa Machi 31, amesema aliishi katika woga mwingi kila sekunde akihofia naye atauawa hivyo.Picha: Ben Curtis/picture alliance/AP Photo

Corinne Dufka, mkurugenzi mtendaji wa haki za binadamu wa Human Rights Watch katika kanda ya Sahel amesema ukiukwaji haki unaofanywa na wanamgambo si sababu tosha kuruhusu jeshi kuwaua watu ambao wamekamatwa tayari. Ameongeza kuwa serikali ya Mali inawajibika kuhusu dhuluma hizo.

Shirika la Human Rights Watch lilizungumza na watu 27 ambao wanafahamu mengi kuhusu mauaji hayo, miongoni mwao mashuhuda kutoka Moura, wafanyabiashara, viongozi wa jamii, wanadiplomasia na wachambuzi wa masuala ya usalama.

Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imeihimiza Mali kufanya uchunguzi huru kuhusu ripoti hiyo kwamba jeshi lake kwa ushirikiano na jeshi la Urusi lilifanya mauaji ya kikatili wiki iliyopita.

Katika taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema jenerali mkuu wa jeshi la Mali hakutaja kuuawa kwa raia katika taarifa yake ya awali, hali inayokinzana na kauli za mashuhuda waliosema raia waliuawa.

Mnamo Februari, Ufaransa ilitangaza kuwaondoa wanajeshi wake nchini Mali kufuatia kuvunjika kwa uhusiano mwema na jeshi linalotawala baada ya mapinduzi ya kijeshi.
​​Mnamo Februari, Ufaransa ilitangaza kuwaondoa wanajeshi wake nchini Mali kufuatia kuvunjika kwa uhusiano mwema na jeshi linalotawala baada ya mapinduzi ya kijeshi.Picha: AP Photo/picture alliance

Ufaransa vilevile imesema imesikitishwa mno na ripoti ya mauaji ya raia yaliyofanywa na jeshi la Mali Pamoja na washirika wake, hususan wanajeshi wa kampuni binafsi ya Urusi Wagner.

Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa pia imesisitiza kuwa vita dhidi ya ugaidi katika kanda ya Sahel havipaswi kutumiwa kwa vyoyvote vile kama sababu ya kukiuka haki za binadamu.

Kauli kama hiyo ya kusikitishwa na inazozusha wasiwasi pia imetolewa na Umoja wa Ulaya kupitia mkuu wake wa sera za kigeni Josep Borrell, akilitaka taifa hilo la magharibi mwa Afrika kuwaruhusu wachunguzi kufika katika eneo hilo.

Mali ambayo ni taifa lenye watu milioni 21 imekuwa ikipambana na wanamgambo walioibuka mwaka 2012, na kusambaa katika mataifa mengine Jirani kama Burkina Faso na Niger.

Katika tukio jingine, wakuu wa serikali ya Mali wamemtaka kiongozi wa upinzani Oumar Mariko kujiwasilisha mbele yao pamoja na watu wa familia yake na afisa wake wa usalama. Hii ni baada ya Mariko kuukosoa utawala wa kijeshi na kudai jeshi linawaua raia.

Chama cha Mariko SADI kilisema Jumatatu kwamba idadi kubwa ya watu waliokuwa na silaha walivamia makaazi ya mwansiasa huyo na kuwataka jamaa zake waeleze wapi aliko.

(HRW, Afp, Rtrs)