1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Kufukuzwa kwa Wamasai huko Loliondo kumekiuka haki zao

27 Aprili 2023

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch lisema kitendo cha serikali ya Tanzania kuwafurusha jamii za Wamasai kutoka maeneo yao ya asili kinakiuka haki zao za kuishi na kumiliki ardhi.

https://p.dw.com/p/4QcT4
Maasai aus Loliondo in Tansania
Picha: Judith Fehrenbacher

Shirika hilo la Human Rights Watch limesema tangu mwezi Juni mwaka 2022, mamlaka nchini Tanzania zimejihusisha na vitendo vya unyanyasaji na vilivyo kinyume cha sheria ikiwa ni pamoja na kupiga, kufyatua risasi, unyanyasaji wa kingono, na ukamataji kiholela ili kuwaondoa wakazi hao kwa nguvu kutoka katika ardhi yao.

Serikali ilitangaza Juni 6, 2022  kuwa itatenga eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,500 za kijiji kuwa eneo la hifadhi na kuwazuia wafugaji ambao ni wakazi wa tarafa ya Loliondo, wilayani Ngorongoro, kuishi kwenye eneo hilo kwa malisho ya mifugo au hata kuingia eneo hilo kutafuta maji kwa matumizi ya kaya na kilimo.

Jamii hiyo ya Wamasai wameiambia Human Rights Watch kuwa hawakushauriwa vya kutosha kabla ya uamuzi huo, kama inavyotakiwa na sheria za Tanzania.

Human Rights Watch | Logo
Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch (HRW)Picha: John MacDougall/AFP/Getty Images

Oryem Nyeko, mtafiti kuhusu Tanzania katika shirika la Human Rights Watch amesema kitendo cha kuhamishwa kwa Wamasai kutoka katika ardhi yao ya asili kimekuwa na athari mbaya na kunauweka hatarini utamaduni wao. Ameendelea kusema kuwa serikali inapaswa kuacha kunyakua ardhi ya Wamasai na ifuate mfumo wa uhifadhi unaoheshimu haki za jamii zilizoathirika.

Soma pia: Mahakama ya EAC yajiandaa kwa rufaa ya Loliondo

Kati ya mwezi Juni na Desemba mwaka 2022, Shirika la Human Rights Watch liliwahoji watu 45, wakiwemo wahasiriwa wa ghasia na vitisho kutoka kwa vikosi vya usalama vya serikali ya Tanzania pamoja na walinzi wa hifadhi za wanyamapori ambao siku mbili tu baada ya tangazo la serikali, waliwasili Loliondo kwa ajili ya kutekeleza agizo la serikali.

Kwa muda wa siku kadhaa, vikosi hivyo viliwakamata na kuwaweka kizuizini viongozi 10 wa jamii za Wamasai huku wakiwafyatulia waandamanaji mabomu ya machozi na risasi za mpira. Takriban watu 30, wakiwemo wanawake, watoto na wazee walijeruhiwa.

Mashuhuda walisema polisi walimchukua kutoka nyumbani kwake mzee mwenye umri wa miaka 84 ambaye hadi sasa haijulikani aliko tangu wakati huo. Vikosi vya usalama pia viliharibu mali za wakaazi, kuwapiga risasi na kuua mifugo yao. Hadi wakazi 2,000 kutoka vijiji mbalimbali vya Loliondo walilazimika kukimbia kutafuta hifadhi na matibabu katika nchi jirani ya Kenya.

Maasai aus Loliondo in Tansania
Wamasai huko Loliondo nchini Tanzania wakitetea haki yao Picha: Judith Fehrenbacher

Tangu wakati huo, vyombo vya ulinzi na usalama vimeendelea kufanya dhuluma dhidi ya wakazi wa Loliondo, huku wahanga na mashahidi wakiendelea kusimulia matukio kadhaa ya ubakaji na ukatili mwingine wa kijinsia, uvamizi wa usiku na kupigwa risasi majumbani.

Soma pia: Asasi za kiraia kutoridhishwa na tathmini kuhusu Loliondo

Serikali ya Tanzania imekuwa ikikana kuwepo kwa jamii za watu wanaoishi eneo hilo na kudai kwamba hatua yao ya kuzuia ufikiaji wa eneo hilo ni kwa lengo la kulinda mazingira katika eneo zima la Serengeti na kutangaza kwamba hatua hiyo ina manufaa makubwa zaidi.

Wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu waliitaka Tanzania kukomesha vitendo vya kuwafukuza watu huko Loliondo. Mwezi Januari 2023, Tume ya Afrika ilitembelea wilaya ya Ngorongoro na kuibua wasiwasi kuhusu kukosekana kwa mashauriano ya kutosha na ushirikishwaji wa jamii husika katika zoezi la uwekaji mipaka na matumizi ya nguvu pamoja na vitisho dhidi ya wanajamii wanaoandamana. 

(Chanzo: HRW)