IAEA yatoa onyo kuhusu kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia
6 Machi 2024Grossi alikuwa akijibu pendekezo la shirika la usimamizi wa nyuklia la Urusi kwamba kinu hicho kianze kutumika tena.
Grossi ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hatua hiyo sio ya kuchukuliwa hivi karibuni na kwamba amekuwa akiwaeleza wenzake wa Urusi ukweli kwamba hatua yoyote kama hiyo inahitaji kuzingatia masuala kadhaa.
Kwanza kabisa, Grossi amesema kuwa eneo hilo ni uwanja wa mapigano na pili, shughuli katika kinu hicho zimesimamishwa kwa muda mrefu.
Soma pia: IAEA yamezuiwa kufika maeneo ya kiwanda cha Zaporizhzhia
Grossi hakufutilia mbali mpango wa kufunguliwa tena kwa kinu hicho cha nyuklia katika siku za baadaye lakini amesema, kutahitajika kufanywa tathmini kadhaa za kiusalama.
Kinu cha Zaporizhzhia kilichotekwa na Urusi katika siku za mwanzo za vita vyake nchini Ukraine, kimefungwa tangu mwaka 2022 kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya makombora.