Idadi ya vifo yaongezeka hadi 41 kufuatia shambulio Kongo
9 Juni 2024Msemaji wa jeshi la Kongo katika jimbo la Kivu Kaskazini Luteni Kanali Mak Hazukay amesema shambulio hilo lilifanywa na waasi wa ADF.
Afisa wa eneo hilo Fabien Kakule ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa watu waliojihami walitumia bunduki na mapanga kuwashambulia wanakijiji katika eneo la Beni.
Soma pia: Zaidi ya raia 50 wauawa na ADF mashariki mwa DRC
Naye Kiongozi wa shirika la kiraia Vusindi Nick Junior amesema kituo cha afya katika eneo hilo kiliteketezwa kwa moto huku watu wengine tisa wakijeruhiwa, kando na 41 waliouawa.
Waasi wa ADF wenye mafungamano na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu wanaendesha harakati zao mashariki mwa Kongo na wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara, na kuyumbisha eneo hilo la mashariki lenye makundi kadhaa ya wapiganaji.
Waasi hao ambao wanatokea nchi jirani ya Uganda wanadaiwa kuhusika pia na shambulio lengine lililosababisha vifo vya watu 16 wiki iliyopita.