Idadi ya waliofariki kutokana na kimbunga Freddy yafika 100
14 Machi 2023Kimbunga hicho ambacho kinatajwa kuwa moja kati ya dhoruba kali zaidi kuwahi kurekodiwa, kilipiga maeneo ya Kusini mwa Afrika mwishoni mwa wiki hadi kuelekea jana Jumatatu.
Kulingana na shirika la hali ya hewa duniani, kimbunga Freddy kinaweza pia kuvunja rekodi ya kimbunga cha tropiki kilichodumu kwa muda mrefu zaidi. Aidha kilitangazwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwezi Februari.
Malawi ndio nchi iliyoathirika zaidi na kimbunga hicho, ambapo hadi sasa watu 99 wamepoteza maisha yao kufuatia maporomoko ya udongo yaliyosomba nyumba kadhaa nchini humo.
Soma pia: Kimbunga Batsirai chasababisha vifo vya watu sita Madagascar
Kamishna katika idara ya kukabiliana na majanga Charles Kalemba amewaambia waandishi wa habari kuwa, wanatarajia idadi hiyo kuongezeka.
Kalemba ameeleza kuwa, watu 134 wamejeruhiwa na wengine 16 hawajulikani waliko. Tayari mji mkuu wa kibiashara wa Malawi Blantyre umerekodi vifo 85 viliyotokana na kimbunga hicho.
Shughuli za uokozi zingali zinaendelea huku wakaazi wakiripotiwa kutumia mikono yao kuchimba wakiwa na matarajio ya kupata manusura zaidi.
Waokoaji wa serikali waliwasili kuchelewa katika eneo la tukio, wakati mkaazi mmoja aliyekataa kutaja jina lake na akiwa amefunikwa na tope, akiendelea na zoezi la uokoaji.
Aubrey Singenyama, naibu msemaji wa polisi katika mji mkuu Blantyre amesema, "Tunazipeleka maiti kila tunapozipata katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali Kuu ya Malkia Elizabeth ambayo kwa sasa imejaa. Licha ya hivyo, tutaendelea kupeleka maiti zaidi iwapo tutazipata.”
UN: Zaidi ya watu 11,000 wameathirika na dhoruba hiyo
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu 11,000 wameathirika na dhoruba hiyo.
Athari ya kimbunga hicho kinaonekana kutonesha kidonda na kuongeza mzigo kwa taifa hilo ambalo tayari linakabiliana na mripuko mbaya wa kipindupindu. Ugonjwa huo wa kuharisha umewauwa zaidi ya watu 1,600 tangu mwaka jana.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia watoto UNICEF limetahadharisha kuwa, hali mbaya ya hewa kama hiyo iliyosababisha kimbunga, inaweza kuzidisha kuenea kwa magonjwa yatokanayo na maji chafu au kwa kunywa maji yasio salama kama vile kipindupindu.
Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ambaye kwa wakati huu anahudhuria mkutano wa mataifa yanayoendelea unaofanyika mjini Doha, Qatar, ametangaza dhoruba hiyo kuwa janga la kitaifa.
Serikali imetoa wito wa msaada wa ndani na kimataifa ili kuwasaidia wahanga wa kimbunga hicho.
Soma pia:Kimbunga "Jobo" kupiga Pwani ya Tanzania na Zanzibar
Malawi imeamuru shule katika wilaya 10 za kusini mwa taifa hilo zifungwe hadi siku ya Jumatano, huku mvua na upepo mkali ukitarajiwa kupiga maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.
Ama kwa upande wa nchi jirani ya Msumbiji, mamlaka imesema takriban watu 10 wamekufa na wengine 14 wamejeruhiwa.
Taasisi ya kitaifa ya kukabiliana na majanga nchini humo imeeleza kuwa, athari ya kimbunga Freddy ilikuwa mbaya zaidi kuliko ilivyotarajiwa.
Kwa ujumla, kimbunga Freddy hadi sasa kimegharimu maisha ya watu wasiopungua 136- 99 nchini Malawi, 20 nchini Msumbiji na watu 17 nchini Madagascar.
Vimbunga vya mwisho kuwahi kuvuka kusini mwa Bahari ya Hindi vilikuwa Leon-Eline na Hudah mnamo mwaka 2000.