Mafuriko makubwa yaikumba tena Msumbiji
28 Aprili 2019Mamia kwa maelfu ya raia nchini Msumbiji wanakabiliwa na kitisho kikubwa, katika wakati ambapo mamlaka ya hali ya hewa imetahadharisha kuhusu mvua kubwa zaidi katika siku zijazo.
"Tusaidieni jamani, tunapoteza kila kitu" amelalama raia mmoja katika mji wa Pemba pembezoni mwa magari yaliyokuwa yanapita wakati maji yalipokuwa yakiingia kwa nguvu kwenye nyumba zao huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha.
Wanawake na wasichana waliokuwa na ndoo na masufuria walikuwa wakijaribu kuzuia maji bila ya mafanikio kwa kuwa yaliendelea kuingia ndani.
Kulingana na watumishi wa Umoja wa Mataifa nyumba zilikuwa zimeanza kuanguka na vikosi vya uokozi vilikuwa vinahamasishana kuanza kuwasaidia raia. "Kwa bahati mbaya tunatarajia mafuriko makubwa" shirika la misaada ya kiutu la Umoja wa Mataifa liliandika kwenye ukurasa wake wa twitter.
Kimbunga Kenneth kimeipiga Msumbiji wiki sita tu baada ya kimbunga kikubwa Idai kilichopiga eneo la kati la nchi hiyo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 600 kutokana na mafuriko makubwa.
Kulingana na Umoja wa Mataifa mvua za kimbunga Kenneth huenda zikawa nyingi mara mbili zaidi ya zile za Idai.
Kiasi cha milimita 250 ama kiasi robo ya wastani wa mvua za mwaka mzima kwenye eneo hilo zinatarajiwa kunyesha kwa siku chache zijazo.
"Sijawahi kuona mvua kama hizi maishani mwangu" amesema Michael Fernando mwenye miaka 35 raia wa Pemba. "Tutaendelea kutembea hadi tutakapofika mahali palipo salama" raia mmoja alisema, wakati watu wakiwa wanakimbia wakiwa wamebeba vitu vyao kwenye mfuko ya plastiki.
Baadhi ya raia wa Pemba walijaribu kupanga matairi na mifuko ya mchanga kuzuia maji. Watoto walijificha kwenye basi lililokuwa limekwama huku magari mengine yakipita kwa shida barabarani na mengine yalianza kuteleza kutokana maji mengi yaliyokuwa yakimwagika barabarani.
Hii ni mara ya kwanza katika historia, kwa taifa hilo la kusini mwa Afrika kukumbwa na vimbunga viwili hali ambayo kwa mara nyingine inaibua wasiwasi kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Takriban watu 700,000 huenda wakakabiliwa na kitisho na hususan katika maeneo ya vijijini, wengi wao wakiwa katika hatari ya kufikwa na njaa.