1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IGAD kufanya mkutano wa dharura kuhusu Tigray

14 Desemba 2020

Waziri Mkuu wa Sudan amesema amekubaliana na mwenziwe wa Ethiopia kufanya mkutano wa dharura, utakaojumuisha mataifa yalio katika Shirikisho la Maendeleo la Pembe ya Afrika IGAD, utakaohusu utatuzi wa mzozo wa Tigray.

https://p.dw.com/p/3mfcd
Äthiopien Abiy Ahmed
Picha: Amanuel Sileshi/AFP

Hata hivyo pamoja na jitihada za Shirika la Habari la Ufaransa AFP, upande wa pili wa ofisi ya waziri mkuu wa Ethiopia haikuweza kupatikana kutolea ufafanuzi tangazo la Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok. Jana, Jumapili Hamdok amekwenda Addis Ababa kwa lengo la kuujadli mzozo wa Tigray, na Waziri Mkuu wa Abiy Ahmed, ikiwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kuitembelea Ethiopia, tangu kuzuka kwa mapigano Novemba 4, ambayo yamezusha janga la kibinaadamu.

Ofisi ya Hamdok ilisema ziara hiyo inaongozwa na mazungumzo yenye tija na kwamba imekubaliwa kufanyika kwa mkutano wa dharura wa mataifa yalio katika Shirikisho la Maendeleo la Pembe ya Afrika IGAD. Shirikisho hilo lililoanzishwa 1996, linayakutanisha mataifa ya Afrika Mashariki ambayo ni Ethiopia, Sudan, Djibouti, Kenya, Somalia, Sudan Kusini na Uganda.

Matokeo ya mkutano wa mawaziri wakuu Hamdok na Abiy Ahmed

Tigray-Konflikt | Militär Äthiopien
Wanajeshi wa serikali ya EthiopiaPicha: Ethiopian News Agency/AP/picture alliance

Maafisa wa serikali ya Sudan waliliambia shirika la habari la AFP kwamba, mkutano wa Hamdok na Abiy umekuwa wenye tija, na hasa katika hatua ya kufanyika mkutano wa dharura wa IGAD, pamoja na kufufua kamati ya pamoja inatakayoshughulikia kero za katika maeneo yao ya mipaka.

Abiy, ambae ni mshindi wa Tuzo ya Nobeli ya mwaka uliopita, amekuwa mkaidi dhidi ya mashinikizo ya kutaka mazungumzo ya amani ya jumuiya ya kimataifa la majuma kadhaa, yakiwemo ya Marekani, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.  Kwa upande wake Abiy, alisema Hamdok katika mazungumzo ya ana kwa ana alionesha uungaji mkono katika mashambulizi dhidi ya Wapiganaji wa Chama cha Ukombozi cha watu wa Tigray, TPLF na kampeni yake ya kuwapokonya silaha.

Soma zaidi:Misaada yawasili kwa mara ya kwanza katika jimbo la Tigray

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu huyo wa Ethiopia inaeleza "upande wa Sudan umeonesha uungaji mkono kwa serikali ya Ethiopia, katika jitihada zake za kusimamia utekelezwaji wa sheria za nchi."

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa lenye kushughulikia migogoro, ICG, maelfu wameuwa tangu kuzuka kwa mapigano katika jimbo la Tigray,  na wengine zaidi ya 50,000 wamekimbilia taifa jirani la Sudan, na hiyo ikiwa ni baada ya Waziri Mkuu Abiy, aamrishe jeshi kwenda kukabiliana na wapinzani wa chama tawala.

Chanzo: AFP