Misaada yawasili kwa mara ya kwanza katika jimbo la Tigray
12 Desemba 2020Shirika la ICRC limesema malori saba ya Shirika hilo la Msalaba Mwekundu yamepeleka shehena ya madawa na vifaa vya matibabu kuwasaidia watu wapatao 400 waliojeruhiwa na vifaa vingine ni kwa ajili ya vituo vya afya. Idara ya wagonjwa mahututi, ICU, na vyumba vya upasuaji vilifungwa kutokana na ukosefu wa vifaa vya matibabu na umeme.
Serikali kuu ya Ethiopia ilizuia kuingia katika mkoa wa Tigray mara baada ya mapigano kuanza mnamo Novemba 4 kati ya serikali kuu na utawala wa jimbo hilo. Maalfu ya watu wanahofiwa kuwa wamekufa kwenye mgogoro huo na wengine wapatao 950,000 wameyakimbia makazi yao.
Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kutoa misaada bado hayajaweza kufikisha misaada katika jimbo hilo. Hata hivyo serikali imesema imepeleka chakula na mahitaji mengine baada ya kuvidhibiti vikosi vya utawala wa zamani wa jimbo hilo chini ya chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) na kufikia makubaliano na Umoja wa Mataifa ambayo yameruhusu misaada kuingia jimboni humo.
Soma zaidi: UN: Hali ya Ethiopia inahitaji uangalizi wa dharura
Kwa wiki kadhaa jumuia ya kimataifa imekuwa ikitoa wito kwa serikali ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed wa kuingizwa misaada katika jimbo la Tigray.
Mashirika mengine ya misaada na wafadhili wanasema makubaliano hayo yameandamana na vizuizi chungunzima na pia hali ya usalama hairidhishi kwa kutolea mfano wa afisa mmoja wa usalama wa Umoja wa Mataifa aliyepigwa risasi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mashirika hayo ya misaada yanahofia uwezekano wa kutokea janga la kibinadamu kwenye jimbo hilo ambapo wakimbizi wa Eritrea nao wamejikuta katikati ya mzozo huo.
Angalia:
Karibu wakimbizi 50,000 wamevuka na kuingia mashariki mwa Sudan tangu mapema mwezi Novemba. Karibu wakimbizi 15,000 wako katika kambi ya Um Rakuba.
Vyanzo: AFP/RTRE