1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMF yataka Afrika isaidiwe kukabiliana na corona

18 Aprili 2020

Maambukizi ya virusi vya corona kote ulimwenguni yamepindukia milioni 2.18 na watu zaidi ya 147 elfu wamepoteza maisha. Sasa Shirika la Fedha Duniani IMF limetoa wito wa msaada wa haraka wa kimataifa kwa nchi za Afrika.

https://p.dw.com/p/3b5xq
Kenia | Coronavirus

Kenia | Coronavirus
Picha: Getty Images/AFP/L. Tato

IMF, pamoja na viongozi wa Afrika na Benki ya Dunia wametoa wito huo wakati ambapo janga hilo linatarajiwa kusababisha uchumi wa bara hilo kushuka kwa asilimia 1.25 mwaka huu wa 2020.

Mkurugenzi mkuu wa IMF Kristalina Georgieva amewaambia mawaziri, maafisa wa Umoja wa Mataifa na wengine kwamba bara la Afrika halina raslimali za kutosha na miundo mbinu ya kutosha ya afya ili kukabiliana na janga hilo na kwamba linahitaji karibu dola bilioni 114. Katika mkutano wa msimu wa machipuko wa Benki ya Dunia na IMF uliofanyika kwa njia ya video, maafisa wameelezwa kuwa licha ya ahadi zilizotolewa bado kuna mapungufu za dola bilioni 44.

Huenda nchi nyingi zikaangazia idadi ya vifo vitokanavyo na corona

Umoja wa Mataifa unasema ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona unatarajiwa kusababisha vifo laki tatu katika bara la Afrika.

Coronavirus Mosambik Maputo NGOs informieren über Covid-19
Mashirika yasiyo ya kiserikali yakihamasisha jamii kuhusu corona huko MaputoPicha: DW/Romeu da Silva

Huku hayo yakijiri, Shirika la Afya duniani WHO limesema huenda nchi nyingi zikaufuata mkondo wa China na kuangazia upya idadi ya vifo katika nchi zao mara tu watakapofikia hatua ya kulidhibiti janga hili. Wuhan, mji ambao ndio uliokuwa kitovu cha virusi vya corona umekiri kwamba kulikuwa na mapungufu katika hesabu ya vifo iliyotolewa awali na ghafla uongozi eneo hilo ukaongeza idadi ya waliofariki kwa asilimia hamsini. Haya yanakuja wakati ambapo ulimwengu una mashaka kuhusiana na hesabu za China kuhusiana na mripuko huo. Awali Wuhan ilijaribu kuficha mripuko wa virusi hivyo kwa kuwaadhibu madaktari waliotoa taarifa za awali kuhusiana na virusi hivyo mitandaoni.

Huenda watu 40,000 wakafariki Uingereza

Na huko Marekani, huku nchi hiyo ikiwa inaongoza kwa visa vya maambukizi na vifo kote duniani kwa sasa gavana wa mji wa New York ambao ndio kitovu cha virusi hivyo Marekani, Andrew Cuomo, ameendelea kushambuliana na Rais Donald Trump huku akisema kuwa Trump anaelekeza lawama kwa majimbo tofauti sasa na kwamba lengo lake kuu ni biashara kuliko jamii zilizoathirika zaidi. Haya ni baada ya Trump kusema kuwa hivi karibuni, atalegeza vikwazo vilivyoko sasa hivi ili kuunusuru uchumi wa Marekani.

USA Corona-Pandemie Andrew Cuomo
Gavana wa jimbo la New York, Marekani, Andrew CuomoPicha: picture-alliance/dpa/J. Minchillo

Na huko Uingereza, profesa mmoja mkuu wa afya ya umma amewaambia wabunge kuwa huenda karibu watu 40,000 wakafariki dunia nchini humo kwa kuwa Uingereza ilichukua muda mrefu kuchukua hatua za kukabiliana na mripuko wa virusi vya corona.

Mashariki ya Kati nako uongozi mkuu wa dini ya Kiislamu Saudi Arabia umesema iwapo mkurupuko wa corona utaendelea basi Waislamu watalazimika kusalimu nyumbani wakati wa mfungo wa Ramadhani na hata sikukuu ya Iddi.

Wakati huo huo Dubai, imeongeza kwa wiki moja marufuku yake ya kutotoka nje kwa siku nzima yaliyowekwa ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.