1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran yazishutumu nchi za kigeni kwa machafuko yanayoendelea

17 Novemba 2022

Kamanda wa kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, Hossein Salami amezishutumu nchi za kigeni kwa kupanga njama za kuanzisha vita kwenye nchi hiyo ambayo imekumbwa na maandamano makubwa ya kuipinga serikali.

https://p.dw.com/p/4JfRW
Iran | Hossein Salami, Kommandeur der iranischen Revolutionsgarde
Picha: SalamPix/abaca/picture alliance

Akizungumza Alhamisi katika mji wa kaskazini wa Qom, Salami amesema maadui wa Iran wanaandaa vita. Kamanda huyo wa jeshi ameenda mbali na kuzitaja Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Israel na Saudi Arabia kama ''mashetani ya ulimwengu.'' Salami amesema hiyo ni njama kubwa dhidi ya taifa hilo na baadhi ya watu ndani ya nchi wamekuwa vibaraka wa maadui wao kwa kuliharibu taifa la Iran.

Hivi karibuni, Umoja wa Ulaya ulimuwekea Salami vikwazo kutokana na Iran kuipatia Urusi silaha wakati ambapo nchi hiyo imeivamia Ukraine.

Maandamano makubwa ya Jumatano

Umati mkubwa wa watu uliendelea kuandamana katika mitaa mbalimbali ya Iran jana Jumatano. Wanaharakati walikuwa wameitisha maandamano ya siku tatu na mgomo katika kukumbushia ghasia zilizotokea wakati wa ukandamizaji wa serikali dhidi ya maandamano ya mwaka 2019, yanayojulikana zaidi kama ''Bloody November'' ambapo watu wengi waliuawa mwezi huo wa Novemba.

Mamia ya waandamanaji waliuawa wakati huo. Wimbi la maandamano ya hivi karibuni liliibuka miezi miwili iliyopita baada ya kifo cha mwanamke wa Iran, Mahsa Amini. Amini mwanamke wa Kikurdi, alikamatwa na polisi wa maadili wa Iran katikati ya mwezi Septemba kwa kukiuka kanuni za mavazi za taifa hilo la Kiislamu. Amini alifariki akiwa chini ya kizuizi cha polisi siku chache baadae, na watu wamekuwa wakihoji sababu ya kifo chake.

Iran Zahedan | Proteste
Wanaume wa Iran wakiwa aktika maandamano kwenye mji wa ZahedanPicha: UGC/AFP

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amirabdollahian amesema mataifa ya kigeni yanapanga njama za kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe katika taifa hilo la Kiislamu ambalo limekumbwa na maandamano makubwa ya kuipinga serikali tangu yalipofanyika mapinduzi ya mwaka 1979. 

Amirabdollahian amesema idara kadhaa za usalama, Israel pamoja na baadhi ya wanasiasa wa mataifa ya Magharibi wamepanga kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe, kuharibu na kuisambaratisha Iran na wanapaswa kujua kwamba Iran sio kama Libya au Sudan.

Maandamano yaungwa mkono na Wairan wote

Iran inawashutumu wapinzani wa nchi za Magharibi kwa kuchochea maandamano ya nchi nzima, ambayo yameungwa mkono na Wairan wote kutoka nyanja tofauti tangu Septemba 16. Siku ya Jumatano, Iran ilikumbwa na mfululizo wa mashambulizi. Watu saba waliuawa katika mji wa kusini magharibi wa Izeh katika kile ambacho vyombo vya habari vya serikali vimelielezea kama shambulizi la kigaidi.

Katika ghasia tofauti, watu wenye silaha waliokuwa wakiendesha pikipiki waliwapiga risasi maaskari kadhaa wa vikosi vya usalama katika mji wa kati wa Isfahan na kuwaua watu wawili na kuwajeruhi wengine wanane. Hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na mashambulizi hayo, ambayo televisheni ya taifa imewatupia lawama waasi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la mahakama ya Mizan, watu watano waliokamatwa wakati wa maandamano hayo, wamehukumiwa adhabu ya kifo. Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International limesema mamlaka ya Iran inataka kutoa adhabu ya kifo kwa watu wapatano 21, katika kesi za uwongo zilizopangwa kuwatisha wale wanaoshiriki katika maandamano hayo.

 

(DPA, AFP, Reuters)