1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Iran:Marekani inataka kutusambaratisha

Mohammed Khelef13 Oktoba 2022

Rais wa Iran ameishutumu Marekani kwa kujaribu kulisambaratisha taifa hilo la Kiislamu, huku watu saba wakiripotiwa kupoteza maisha kwenye maandamano ya usiku ya kuamkia leo ukiwa muendelezo wa maandamano ya mwezi mzima

https://p.dw.com/p/4I9M0
Iran
Picha: Iranian Presidency Office/AP/picture alliance

Rais Ibrahim Raisi anayetambuliwa kuwa mwenye msimamo mkali wa kisiasa amerejela shutuma zake kwamba Marekani, ambayo imekuwa hasimu mkubwa wa Iran tangu mapinduzi ya mwaka 1973, ndiyo inayohusika na machafuko yanayoendelea sasa.

Akizungumza akiwa ziarani nchini Kazakhstan, Raisi amesema  "Kufuatia kushindwa kwao kwenye kampeni za kijeshi na vikwazo, sasa Washington na washirika wake wamegeukia sera iliyoshindwana kupandikiza machafuko."

Marekani, ambayo imeiwekea vikwazo vipya Iran kutokana na maandamano hayo, imesema inachukuwa hatua zaidi kuhakikisha kuwa Wairani wana fursa za kuwasiliana kwa mitandao, baada ya serikali mjini Tehran kuweka vizuizi kwenye matumizi ya intaneti na kupiga marufuku majukwaa ya mitandao ya kijamii, zikiwemo Instagram na WhatsApp.

Soma pia:Watu 31 wauawa kwenye maandamano nchini Iran

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Wendy Sherman, amesema "Ukandamizaji dhidi ya maandamano ya amani ni uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu"

Alisema waziri huyo na kuongeza kwamba amezungumza na kampuni kubwa za teknolojia za Marekani na kuwataka kuwaachia watu wa Iran huduma za ziada na nyenzo za mawasiliano.

Kifo cha Mahsa Amin chavuruga utulivu Iran

Vuguvugu hili lililoanza kwa maandamano ya wanawake walioghadhabishwa na kifo cha Mahsa Amini aliyefariki dunia siku tatu baada ya kukamatwa na polisi ya maadili mjini Tehran, limeanza kuchukuwa muelekeo wa uasi wa umma, ambapo waandamanaji wanakabiliana na vyombo vya usalama uso kwa uso.

Frankreich | Solidarität für iranische Demonstranten in Paris
picha ya Mahsa Amin ikionesha na mwanamanaji huko IranPicha: Aurelien Morissard/AP/picture alliance

Katika maandamano ya usiku wa kuamkia leo, vyombo vya usalama vilitumia risasi na mabomu ya machozi kukabaliana na waandamanaji maeneo kadhaa nchini Iran kwa mujibu wa makundi ya haki za binaadamu.

Video zilizotumwa mtandaoni zinaonesha raia wakikabiliana na maafisa wa usalama waliokuwa wanataka kuwatia nguvuni bila mafanikio.

Soma pia:Polisi Iran yaendeleza ukandamizaji wa maandamano

Taarifa kutoka mikoa inayokaliwa na Wakurdi zinasema watu saba waliuawa kwenye maandamano ya jana usiku, na kuifanya idadi ya waliokwishapoteza maisha tangu maandamano kuanza wiki nne zilizopita kufikia 200.

Katika mji mkuu wa jimbo la Kurdistan, Sanandaj, shirika la habari la Reuters limeripoti kampeni ya nyumba kwa nyumba inayofanywa na vyombo vya usalama kuwasaka na kuwakamata vijana wanaoshukiwa kuchochea ghadhabu za umma dhidi ya serikali.

Shirika la haki za binaadamu liitwalo Hengaw linasema waandamanaji katika miji kumi ya jimbo hilo wamekabiliana na vyombo vya usalama usiku wa jana. Maafisa watatu wa vyombo vya usalama pamoja na kijana mmoja waliuawa kwenye mji wa Kermanshah.