1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi Iran, wafanyakazi wakaidi ukandamizaji

10 Oktoba 2022

Waandamanaji nchini Iran wameendelea kukalia maeneo huku baadhi ya wafanyakazi wa viwandani wakigoma licha ya ukandamizaji ambao wanaharakati wanasema umesababisha vifo vya makumi ya watu na mamia wengine kujeruhiwa.

https://p.dw.com/p/4I0dn
Iran Protest l Aktivisten hacken Staatsfernsehen
Picha: @EdalateAli1400/Twitter/AFP

Picha za Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zimeashiria kuongezeka kwa maandamnao katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu Tehran na miji mingine katika siku za karibuni, ambapo wanawake wameonekana wakichoma mitandio yao na kutoa kauli za kuupiga utawala nchini humo.

Shirika la haki za binadamu la Kikurdi la Hengaw, limezituhumu mamlaka kwa kutumia silaha nzito, ikiwemo mashambulizi dhidi ya viunga na bunduki za rasharasha, katika mji wa kaskazini-mashariki wa Sanandaj, madai ambayo hata hivyo hayakuweza kuthibitishwa kwa uhuru, katikati mwa uzuwiaji mkubwa wa mawasiliano ya intaneti.

Iran | Ausschreitungen in Teheran
Pikipiki ikiwaka moto mjini Tehran, Oktoba 8, 2022, wakati wa maandamano yanayoendelea kuitikisa Iran kufuatia kifo cha Mahsa Amini.Picha: AFP/Getty Images

Shirika hilo lenye makao yake nchini Norway, limesema milio ya risasi ilisikika pia katika mji wa Saqqez ambako ni nyumbani wa Amini.

Soma pia: Iran yawataka wageni kuheshimu sheria

Machafuko hayo yalizuka zaidi ya tatu zilizopita kuhusiana na kifo cha Mahsa Amini, mwanamke raia wa Iran wa jamii ya Kikurdi aliekuwa na umri wa miaka 22, ambaye alifariki dunia baada ya kukamatwa na polisi wa maadili mjini Tehran.

Wanaharakati wanasema alipigwa akiwa kizuwizini, huku maafisa wa serikali ya Iran wakitoa ripoti ya madaktari inayosema kifo chake kilitokana na hali aliokuwa nayo.

Waandamanaji wameelekezea hasira zao kupitia baadhi ya wanawake wa Kiiran kuhusiana na uvaaji wa laazima wa mitandio, lakini pia zimesikika sauti za kuupinga mfumo wa Kiislamu ulioanzishwa na kiongozi wa mapinduzi Ayatollah Ruhollah Khomeini, baada ya kuupindua utawala wa Shah mnamo mwaka 1979.

Ayatollah awashtumu wengine kwa machafuko

Shirika la haki za binadamu la Iran, IHR, lenye makao yake mjini Oslo lilitoa picha za mgomo katika chuo kikuu cha kaskazini cha Gilan, na wasichana wa sekondari katika mji wa kaskazini wa Mahabad wakivua mitandio yao.

Kundgebung Protest Iran Mahsa Amini in Den Haag
Mwandamanaji akibeba picha ya Mahsa Amini, wakati malelfu walipoonesha uungwaji wao mkono kwa waandamanaji nchini Iran Oktoba 8,2022.Picha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Pia lilichapisha vido ambayo lilisema ilionyesha kundi kubwa la wanafunzi nje ya chuo cha ufundi mjini Tehran, wakilaani umaskini na rushwa nchini Iran, huku wakipiga kelele cha kifo cha udhalimu huu.

Soma pia: Raia wa Iran waendelea kuandamana licha ya onyo la Mahakama

Kwa mujibu wa IHR, watu wasiopungua 185, wakiwemo watoto wasiopungua 19, wameuawa katika maandamano hayo ya nchi nzima. Idadi kubwa zaidi ya mauaji imetokea Sistan na mkoa wa Baluchistan, ambako nusu ya vifo imerekodiwa.

Maelfu ya wanaharakati, waandishi habari na wanafunzi wa vyuo vikuu wamekamatwa pia, lakini maandamano yanaonekana kuendelea bila kusita.

Wakati huo huo, kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amezilaumu Israel na Marekani, na wale aliodai wanalipwa na mataifa hayo, na baadhi ya Wairan wasaliti waishio nje ya nchi, kwa kuchochea maandamano yanayoendelea.

Chanzo: Mashirika