1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq yafanya uchaguzi wa bunge, usalama ukiimarishwa

10 Oktoba 2021

Raia wa Iraq wanapiga kura Jumapili kwenye uchaguzi uliopaswa kufanyika mwakani lakini umeharakishwa kufuatia maandamano yaliyodumu miezi mingi kushinikiza mageuzi.

https://p.dw.com/p/41UOh
Irak -  Mustafa al-Kadhimi bei den Parlamentswahlen
Picha: Khalid Mohammed/AA/picture alliance

Uchaguzi huo ni wa pili tangu Iraq ilipotangaza ushindi wa kijeshi dhidi ya kundi la wanamgambo wa Kiislamu takriban miaka minne iliyopita.

Japo wanamgambo hao wamelemewa na hawana nguvu kama zamani, yapo makundi madogomdogo ya wale wanaojiita ‘Dola la Kiislamu' IS ambayo hufanya mashambulizi ya mara kwa mara katika baadhi ya maeneo ya Iraq.

Maafisa wamesema zaidi ya maafisa wa usalama 250,000 wamepelekwa kushika doria katika vituo vya upigaji kura kote nchini Iraq.

Mipaka ya ardhi na anga ya nchi hiyo pia imefungwa wakati uchaguzi ukiendelea kama sehemu ya kuimarisha usalama.

Soma pai: Marekani na Iraq kujadiliana kuhusu vikosi vya jeshi

Vituo vya kura vilifunguliwa mwendo was aa moja asubuhi. Waziri Mkuu Mustafa al.-Kadhimi alipiga kura yake mjini Baghdad na kutoa wito kwa watu kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

”kura yako ina thamani kubwa. Usiikose nafasi hii ya kuleta mabadiliko,” alisema baada ya kupiga kura kwenye hotuba yake kwa raia wa Iraq.

Usalama umeimarishwa Iraq mnamo wakati nchi hiyo ikifanya uchaguzi wa bunge.
Usalama umeimarishwa Iraq mnamo wakati nchi hiyo ikifanya uchaguzi wa bunge.Picha: Ali Makram Gharee/AA/picture alliance

Al-Kadhimi, aliyechukua madaraka Mei mwaka jana, aliuharakisha uchaguzi huo kwa miezi kadhaa kama jibu kwa maandamano ya raia.

Kipindi cha bunge la sasa ambalo lilichaguliwa mwaka 2018, kilitarajiwa kumalizika mwaka 2022.

Mnamo mwaka 2019, kulizuka maandamano makubwa nchini Iraq kutaka serikali ijiuzulu, bunge livunjwe na mfumo mzima wa kisiasa wa ambao umekuwepo tangu uvamizi wa Marekani nchini humo mwaka 2003, ufanyiwe mageuzi.

Waandamanaji pia walishutumu visa vilivyokithiri vya ufisadi pamoja na uhaba wa huduma za msingi ikiwemo umeme.

Siasa imewakatisha tamaa raia wengi wa Iraq. Wanaounga mkono vuguvugu la maandamano  wametoa wito kwa raia kuususia uchaguzi huo. Wanadai kuwa uchaguzi huo hautaleta mabadiliko yoyote katika mamlaka na mfumo ulioko sasa wa kisiasa.

”Kunatarajiwa mabadiliko finyu sana kwenye uchaguzi huu. Wanaotawala wamekita mizizi kwenye mfumo ili wasiondolewe madarakani hivyo wataendelea kukamata mamlaka,” amesema mchambuzi wa siasa nchini humo Farhad Alaaldin.

Uchaguzi wa Iraq umeharakishwa kufuatia maandamano ya wananchi yaliyoanza 2019.
Uchaguzi wa Iraq umeharakishwa kufuatia maandamano ya wananchi yaliyoanza 2019.Picha: Hadi Mizban/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo, Hussain al-Hendawi ambaye ni mshauri wa waziri mkuu amebashiri kwamba idadi kubwa ya wapiga kura itajitokeza.

"Tumefurahishwa na maandalizi mazuri ya uchaguzi pamoja na idadi ya wanaojitokeza,” aliwaambia waandishi wa habari mjini Baghdad na kutoa takwimu maalum.

Takriban wagombea 3,249 wakiwemo wanawake 951 wanawania viti 329 katika bungee hilo. Robo ya viti hivyo vimetengewa wanawake.

Takriban watu milioni 25 wamesajiliwa kama wapiga kura nchini Iraq. Matokeo ya awali ya uchaguzi huo yanatarajiwa kuanzia Jumatatu.

(DPAE)