Nchi tatu za Ulaya zaitambua Palestina kama dola huru
22 Mei 2024Hatua ya nchi hizo inavunja msimamo ulioshikiliwa kwa muda mrefu na nchi za Magharibi kwamba taifa huru la Palestina linaweza tu kupatikana kwa kuyafanikisha mazungumzo ya amani kati ya mamlaka ya Palestina na Israel.
Waziri Mkuu wa Ireland Simon Harris aliwaambia waandishi wa habari kwamba siku ya Jumatano tarehe 21/05/2024 ni siku muhimu na ya kihistoria kwa nchi yake na kwa watu wa Palestina.
Ireland, Norway na Uhispania zilisema zitaitambuwa rasmi Palestina kama dola huru mnamo Mei 28.
Waziri Mkuu wa Norway Jonas Gahr Store amesema amani haiwezi kuwepo katika eneo la Mashariki ya kati iwapo Palestina haitatambuliwa.
Soma Zaidi: Uhispania kuitambua Palestina kama taifa huru
Chama cha Ukombozi wa Palestina, PLO kinachotambulika kimataifa kama ndio mwakilishi pekee halali wa watu wa Palestina, kimepongeza uamuzi wa kihistoria wa leo Jumatano uliotangazwa nchi tatu za Ulaya wa kulitambua taifa la Palestina. Kundi la Hamas linalotawala katika eneo la Ukanda wa Gaza pia limeipongeza hatua hiyo.
Kutokana na hatua hiyo iliyochukuliwa na Norway, Ireland na Uhispania ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Katz Israel, amewaamuru mara moja mabalozi wake kutoka Norway na Ireland kurejea nyumbani. Amesema hatua kama hiyo pia itachukuliwa kwa balozi wa Israel wa nchini Uhispania.
Israel imepinga vikali hatua hiyo, ikisema kuwa ni sawa na ugaidi baada ya kundi la wanamgambo wa Hamas kufanya mashambulizi katika ardhi ya Israel mnamo Oktoba 7 mwaka uliopita.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Israel amezilaumu Norway, Ireland na Uhispania kwa kwa kuchukua hatua ambayo ameiita kuwa inawanyima haki watu walioathiriwa na mashambulizi ya Hamas ya mwaka jana.
Soma Zaidi:Israel yaapa kuendeleza operesheni ya Rafah dhidi ya Hamas
Serikali za Magharibi na Marekani zasemaje
Hata hivyo serikali nyingi za Magharibi ikiwa ni pamoja na Marekanizinasema ziko tayari siku moja kuitambua Palestina kama taifa huru ingawa zimesema hazitafanya hivyo kabla ya makubaliano kufikiwa kuhusu masuala yenye utata kama vile mipaka kati ya Israel na Palestina pamoja na swala linalohusu hadhi ya mji wa Jerusalem.
Vyanzo: AFP/RTRE/AP/DW