1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yaanzisha uvamizi mpya kaskazini mwa Gaza

6 Oktoba 2024

Takriban watu 24 wameuwawa na wengine 93 kujeruhiwa wakati mashambulizi ya anga ya Israel yalipopiga msikiti na shule inayowahifadhi waliokimbia makaazi yao katika Ukanda wa Gaza mapema leo.

https://p.dw.com/p/4lSQw
Gaza - Jeshi la Israel lafanya mashambulizi ya ardhini dhidi ya Hamas
Kifaru cha Israel wakati wa operesheni ya ardhini inayoendelea ya jeshi la Israel dhidi ya kundi la Hamas, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.Picha: Ronen Zvulun/Reuters

Haya ni kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Gaza inayoendeshwa na Hamas.

Maafisa wa afya wa Palestina wameripoti kwamba takriban watu wengine 20 waliuwawa kufuatia mashambulizi ya Jumamosi usiku kaskazini mwa Gaza, baada ya jeshi la Israel kupeleka vifaru vya kivita katika eneo hilo kwa mara ya kwanza baada ya miezi kadhaa.

Soma pia: Jeshi la Israel laamuru watu waondoke kaskazini mwa Gaza

Jeshi la Israel limesema lilifanya lilichokiita "mashambulio mahsusi dhidi ya magaidi" waliokuwa wakiendesha opereshi zao ndani ya Shule ya Ibn Rushd na msikiti wa al-Aqsa katika eneo la Deir al-Balah katikati mwa Gaza.

Aidha jeshi hilo limesema wamezingira eneo la kaskazini mwa Gaza, kutokana na dalili kwamba kundi la wanamgambo wa Hamas linajenga upya nguvu zake katika eneo la Jabaliya.

Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na Ujerumani ni miongoni mwa nchi ambazo zimeorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.