1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yaapa kulipiza kisasi dhidi ya Iran

16 Aprili 2024

Mkuu wa majeshi ya Israel jenerali Herzi Halevi ameapa Israel itajibu mashambulizi ya Iran licha ya rai kutoka kwa viongozi wa dunia ya kuitaka Israel kujizuia kwa kuhofia mzozo mkubwa wa kikanda.

https://p.dw.com/p/4eqGA
Mkuu wa majeshi wa Israel Herzi Halevi
Mkuu wa majeshi ya Israel jenerali Herzi Halevi akizungumza na wanajeshi katika uwanja wa ndege wa Nevatim.Picha: Israeli Army/AFP

Akiwahutubia wanajeshi katika uwanja wa ndege wa Nevatim ambao ulishambuliwa na Iran katika shambulio la Jumamosi usiku, Herzi Halevi amesema watajibu mashambulio hayo bila ya kutoa maelezo zaidi.

"Iran itakabiliwa na matokeo ya vitendo vyake. Tutachagua jibu letu ipasavyo. Jeshi la Israel bado liko tayari kukabiliana na tishio lolote kutoka kwa Iran na washirika wake wa ugaidi tunapoendelea na dhamira yetu ya kulinda Taifa la Israel.”

Kulingana vyombo vya habari vya Israel Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alikutana na baraza lake la mawaziri linaloshughulikia masuala ya vita Jumatatu jioni kujadili hatua zinazofuata.

Soma pia: Ujerumani yamwita balozi wa Iran kufuatia shambulizi Israel

Serikali za Magharibi, zikiwemo zile zilizoiunga mkono Israel kujikinga na mashambulizi ya Iran, zimeonya dhidi ya ongezeko la mgogoro huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron walikuwa miongoni mwa viongozi wanaoitaka Israel kujizuia.

Kwa mujibu wa afisa mkuu wa Marekani rais Joe Biden amemwambia Netanyahu kwamba Washington haitatoa msaada wa kijeshi wa kulipiza kisasi kwa aina yoyote dhidi ya Iran.

Iran itakuwa tayari kujizuia?

Baada ya shambulizi lake la kulipiza kisasi Iran ilisema ingezingatia kwamba suala hilo "limehitimishwa" lakini hali inaweza kubadilika endapo Israel itajibu shambulizi hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amemwambia mwenzake wa China Wang Yi kwamba Iran "iko tayari kujizuia" na haina nia ya kuongeza mvutano zaidi.

Yi amesema inaaminika kuwa Iran inaweza kushughulikia mgogoro huo na kuepusha machafuko zaidi katika eneo hilo.

Soma pia: Israel: Mashambulizi ya Iran hayatapoteza lengo letu Gaza

Marekani imeendelea kuiomba China mshirika wa karibu wa Iran na mnunuzi mkuu wa mafuta yake kutumia ushawishi kwa Tehran ili kudhibiti mivutano katika Mashariki ya Kati.

Waziri wa Mambo ya Nje Wang Yi China na Hossein Amir Abdollahian Iran
Waziri wa Mambo ya Nje Wang Yi China na Hossein Amir Abdollahian Iran wakijadili mgogoro wa mashariki ya kati kupitia njia ya video.Picha: China's Ministry of Foreign Affairs/Xinhua/picture alliance

Katika mazungumzo ya simu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Yoko Kamikawa amesema Japan ina wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel, ambayo yanazidi kuzorotesha hali ya sasa ya Mashariki ya Kati, na inalaani vikali ongezeko hilo.

Kamikawa pia alitaja umuhimu wa uhuru na usalama katika maeneo ya bahari na kutoa wito kwa Iran kuhakikisha usalama wa safari za meli katika bahari ya eneo hilo.

Haya yanajiri huku Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza ikisema kwamba idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza imeongezeka hadi 33,797.

Katika taarifa yake wizara hiyo imedokeza katika saa 24 zilizopita, jeshi la Israel limewaua Wapalestina 68 na kujeruhi wengine 94.