Israel yaendelea kukabiliana na Hezbollah
21 Agosti 2024Kundi hilo la Hezbollah limevurumisha zaidi ya roketi 50 na kuharibu nyumba kadhaa za raia katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel la milima ya Golan. Hezbollah imesema hilo ni jibu kwa shambulio la Israel huko Lebanon usiku wa Jumanne ambalo lilisababisha kifo cha mtu mmoja na kuwajeruhi wengine 19. Jeshi la Israel limesema hivi leo kuwa lilishambulia kwa mabomu ghala la silaha la Hezbollah katika Bonde la Bekaa nchini Lebanon.
Mashambulizi ya leo Jumatano ya Hezbollah yanajiri siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kukutana na wapatanishi wenzake kutoka Misri na Qatar katika juhudi zake za kidiplomasia zinazolenga kufikiwa mkataba wa usitishaji mapigano katika vita vya Gaza.
Hata hivyo Israel na Hamas wamesema kuwa bado kuna changamoto lukuki. Kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina limesema katika taarifa mpya kwamba pendekezo la hivi karibuni zaidi lililowasilishwa ni "tofauti kabisa" na kile walichoafiki hapo awali huku wakiishutumu Marekani kwa kupigia debe "masharti mapya" yanayotolewa na Israel.
Soma pia: Hezbollah yasema wapiganaji wake wawili wameuawa
Katika muendelezo wa juhudi hizo za kusaka makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza, leo Jumatano, Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Marekani Antony Blinken na walijadiliana pia kuhusu hali jumla katika eneo la Mashariki ya Kati.
Iran yaapa kulipiza kisasi mauaji ya Haniyeh
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Mohammed Naeeni amesema Iran bado italipiza kisasi kufuatia mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh aliyeuawa mjini Tehran:
"Muda bado upo, na inawezekana muda wa kusubiri majibu ukawa mrefu zaidi. Kwa sasa Wazayuni wanakabiliwa na hofu inayotokana na hilo. kipindi cha kusubiri, na ukubwa wa mashambulizi kutoka Iran na makundi mengine ya upinzani. Israel wanapaswa kukaa katika hali hii ya wasiwasi. Huenda jibu la Iran lisiwe kama la hapo awali. Ufanisi wa majibu, mpangilio wake na zana zitakazotumiwa huwa havifanani kila wakati."
Soma pia: Blinken ashinikiza kusitishwa mapigano Gaza
Hali katika eneo hilo imezidi kuwa mbaya kutokana na vita vya Gaza, makabiliano kati ya Israel na makundi ya wanamgambo ya Hezbollah ya Lebanon pamoja na mashambulizi ya Wahouthi wa Yemen yanayolenga meli katika bahari ya Shamu. Hapo jana, Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant alisema kwa sasa jeshi la nchi hiyo linahamisha malengo yake kutoka Gaza na kuelekeza nguvu zote katika eneo la mpakani na Lebanon.
(Vyanzo: AP, DPAE, Reuters, AFP)