1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yakubali kusitisha mashambulizi kwa saa kadhaa Gaza

10 Novemba 2023

Israel imekubali kusitisha mashambulizi yake kwa saa kadhaa kaskazini mwa Gaza, hatua ambayo itaruhusu baadhi ya raia kukimbia mapigano hayo.

https://p.dw.com/p/4Yegt
Wanajeshi wa Israel katika ukanda wa Gaza
Wanajeshi wa Israel katika ukanda wa GazaPicha: Ohad Zwigenberg/AP/dpa/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden amekaribisha uamuzi wa Israel wa kusitisha mashambulizi kwa saa kadhaa, hatua ambayo inarasimisha mpango ambao tayari umeshuhudia maelfu ya Wapalestina wakikimbia mapigano kaskazini mwa Gaza.

Biden amesema kusitishwa kwa mashambulizi hayo ni moja ya hatua katika mwelekeo sahihi japo ameeleza kwamba, "hakuna uwezekano" wa kusitisha kabisa mapigano.

Soma pia: Jeshi la Israel lakabiliana na wanamgambo wa Hamas huko Gaza

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Turk ameitolea mwito Israel kuheshimu sheria za vita na kuepuka mashambulizi ya kiholela ya raia.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Amman, Turk ameeleza wasiwasi wake kwamba haki za binadamu za Wapalestina zinapuuzwa katika mashambulizi yanayofanywa na Israel.

Maelfu ya Wapalestina wakimbilia kusini mwa Gaza

Wapalestina wakikimbia kuelekea upande wa kusini mwa Gaza
Wapalestina wakikimbia kuelekea upande wa kusini mwa Gaza Picha: Hatem Moussa/AP Photo/picture alliance

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewasifu wanajeshi wake kwa kile alichokitaja kuwa, "wanafanya kazi nzuri katika uwanja wa mapambano."

Kiongozi huyo amefafanua kuwa, kamwe hakutositishwa mapigano bila ya kuachiliwa huru kwa mateka wa Israel.

Israel ilianzisha oparesheni ya kijeshi dhidi ya kundi la Hamas baada ya wapiganaji wa kundi hilo kufanya mashambulizi mnamo Oktoba 7, na kuwaua watu 1,400, wengi wao wakiwa raia na kuwachukua mateka karibu watu 240.

Israel imeapa kuliangamiza kabisa kundi la Hamas kwa kufanya mashambulizi ya angani na ardhini, mashambulizi ambayo wizara ya afya katika ukanda wa Gaza imesema yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 10,800 wengi wao wakiwa raia na watoto.

Netanyahu ameweka bayana kuwa, Israel haina nia ya kuitawala Gaza.

Waziri Mkuu huyo amekiambia kituo cha televisheni cha Marekani, Fox News, "Hatuna nia ya kuikalia Gaza lakini tunatafuta njia za kuipa maisha bora ya baadaye.”

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: imago images/Xinhua

Wakati hayo yakiarifiwa, Uturuki imefanya maandalizi ya kuchukua Wapalestina waliojeruhiwa na watu wenye magonjwa sugu kutoka Gaza hadi kwenye hospitali zake kwa matibabu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara yake nchini Uzbekistan, Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amesema Uturuki itafanya juhudi kuiongezea Israel shinikizo ili kuhakikisha Wapalestina waliojeruhiwa wanahamishwa kutoka Gaza.

Soma pia: Israel: Nakisi ya dola bilioni 6 kutokana na vita vya Gaza

Uturuki pia imejadiliana na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken juu ya uwezekano wa kuongeza malori ya msaada na kufikia 500 kuelekea Gaza.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani alionekana kuridhia wazo hilo wakati wa mazungumzo na Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Hakan Fidan.

Ankara imeeleza pia utayari wake wa kutoa magari ya kubebea wagonjwa, chakula, maji na dawa kwa Gaza ikiwa ni sehemu ya ushirikiano na mataifa mengine.