Israel: Tutaheshimu uhuru wa kuabudu wakati wa Ramadhani
11 Machi 2024Yoav ametoa kauli hiyo kupitia ujumbe kwa njia ya video akisema kuwa Israel itaheshimu uhuru wa kuabudu sio tu katika eneo la Msikiti wa Al-Aqsa lakini pia maeneo mengine matakatifu yaliyoko kwenye eneo lililonyakuliwa la Jerusalem Mashariki.
Matamshi yake yanatolewa katikati mwa wasiwasi kuhusu vurugu za wakati wa Ramadhan katika Msikiti wa Al-Aqsa, eneo ambalo limekuwa ni kitovu cha ghasia wakati wa mwezi mtukufu katika miaka iliyopita. Eneo hilo pia hutumiwa na Wayahudi na linajulikana kwao kama Mima wa Hekalu.
Wakati wa mfungo wa Ramadhan, maelfu ya waumini wa Kiislamu hukusanyika na kuswali katika eneo hilo. Ijumaa iliyopita, msemaji wa tawi la kijeshi wa kundi la wanamgambo la Hamas, alitoa wito na kuwahimiza watu kuelekea eneo la Al-Aqsa.
Soma: Makabiliano mapya yazuka kwenye msikiti wa al-Aqsa
Ripoti za vyombo vya habari zinasema kwamba Israel inachunguza ikiwa kiongozi wa ngazi ya pili wa kijeshi wa Hamas aliuawa kwenye shambulizi la anga wakati mazungumzo ya kutafuta usitishaji mapigano huko Gaza yakigongana na kuanza kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Ikiwa ripoti za kifo chake zitathibitishwa, zitamfanya Marwan Issa kuwa afisa wa ngazi ya juu kutoka vuguvugu hilo la wanamgambo wa Kiislamu kuuawa na Israel katika vita vya zaidi ya miezi mitano ambavyo vimelidhoofisa eneo la Wapalestina na kuua maelfu ya watu. Na pia huenda ikatatiza juhudi za kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka waliosalia, ingawa kwa mujibu wa Israel mazungumzo yanaendelea kupitia wapatanishi wa Misri na Qatar.
Redio ya jeshi la Israel ilisema vikosi vya nchi hiyo viliishambulia kwa mabomu kambi ya Al-Nusseirat katikati mwa Gaza jumamosi usiku. Jeshi hilo linadai kwamba lilikuwa na taarifa za kijasusi za uwepo wa Issa, ambaye ni kiongozi wa pili wa tawi la kijeshi la Hamas Brigedi za Izz el-Deen al-Qassam. Watu watano wanadaiwa kuuawa kwenye shambulio hilo. Hata hivyo si jeshi la Israel wala maafisa wa Hamas ambao wametoa kauli kuhusu ripoti hizo za vyombo vya habari.
Ripoti kuhusu misaada: Misaada ya kwanza kwa njia bahari yasubiriwa Ukanda wa Gaza
Lakini hapo jana, katika taarifa kuhusu operesheni zake ndani ya saa 24 zilizopita, Israel ilisema kwamba vikosi vyake vilifanikiwa kuwaua wanamgambo kadhaa katikati mwa Gaza, bila kutaja hiyo kambi.
Marwan Issa yuko katika orodha ya juu ya watu wanaosakwa zaidi na Israeli, pamoja na mkuu wa tawi la kijeshi Mohammed Deif na kiongozi wa Hamas wa Gaza Yahya Sinwar, ambao wanaaminika kupanga shambulio la Oktoba 7 ambalo lilianzisha mzozo.