1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramadhani yaanza bila usitishwaji vita Gaza

Sylvia Mwehozi
11 Machi 2024

Mwezi mtukufu wa Ramadhani umeanza leo kwa waumini wa Kiislamu duniani, huku kukiwa hakuna dalili za makubaliano ya usitishaji mapigano kwenye Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4dNn2
Kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan 2024
Waumini wa Kiislamu wakishiriki sala ya jini ya "Tarawih" wakati wa kuanza kwa mfungo wa Ramadhan kwenye eneo la Msikiti wa Al- AqsaPicha: Ammar Awad/REUTERS

Mataifa ya Mashariki ya Kati yametangaza kuanza kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhan, huku Mfalme Salman wa Saudi Arabia akitumia fursa hiyo kutoa wito wa kusitishwa kwa "uhalifu wa kutisha" katika Ukanda wa Gaza.

Soma ripoti hii: Leo ni mwanzo wa mwezi wa Ramadhani kwa Waislamu wengi

Akizungumza kama mlinzi wa maeneo mawili matakatifu ya Kiislamu, Mfalme Salman wa Saudi Arabia alitoa shukrani katika ujumbe wake alioutoa jana jioni kwa "baraka iliyopewa Ufalme wa Saudia Arabia" lakini amebainisha kwamba vita vya Gaza vitatia kiwingu funga na maombi ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

"Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufanya wajibu wake wa kukomesha uhalifu huu wa kutisha na kuhakikisha uanzishwaji wa njia salama za kibinadamu na misaada."

Indonesien | kuanza kwa Ramadhan 2024
Wanawake wa Kiislamu wakiukaribisha mwezi wa Ramadhan katika Msikiti wa At-Taqwa nchini IndonesiaPicha: Riska Munawarah/REUTERS

Wapatanishi wa Marekani, Qatari na Misri wamekuwa wakifanya mazungumzo kwa wiki kadhaayaliyolenga usitishaji wa mapigano kwa muda wa wiki sita na kuachiwa kwa mateka waliosalia kwa mabadilishano ya Israel kuwaachia wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa kwenye jela.

Shinikizo la kidiplomasia

Chanzo kimoja kilicho na ufahamu na mazungumzo hayo, kimeliambia shirika la habari la AFP kwamba "kutakuwa na msukumo wa kidiplomasia ndani ya siku 10 zijazo" kwa nia ya kupata makubaliano katika nusu ya kwanza ya Ramadhan.

Soma: Hamas yasema itaendelea na mazungumzo ya usitishaji vita

Katika ujumbe wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alielezea "mshikamano na kuwaunga mkono wale wote wanaoteseka kutokana na hali ya kutisha huko Gaza. Katika nyakati hizi za majaribu, mfungo wa Ramadhani ni mwanga wa matumaini, ukumbusho wa ubinadamu wetu wa pamoja".

 "Ni kipindi cha kutafakari na sala, fursa ya kukusanyika pamoja na kuinuana. Cha kusikitisha ni kwamba wengi wataadhimisha mwezi huu huku wakikabiliwa na migogoro, kukimbia na hofu," alisema Guterres.

Saudi-Arabia | Kuanza kwa Ramadhan 2024
Maafisa wa Saudia wakitizama kuandamana kwa mwezi ikiashiria kuanza kwa mfungo wa RamadhanPicha: FAYEZ NURELDINE/AFP/Getty Images

 

Usambazaji misaada waendelea

Huku hayo yakiripotiwa, juhudi za kusambaza misaada Gaza zinaendelea.

Meli ya misaada ya Uhispania ilikuwa inaandaa upelekwaji wa misaada kwa njia ya anga kutokea Cyprus kupitia pwani ya Ukanda wa Gaza ambako Umoja wa Mataifa umeonya mara kwa mara juu ya kitisho cha njaa.

Mataifa mengine ya Jordan, Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na Misri nayo yalidondosha misaada ya kiutu Kaskazini mwa Ukanda wa Gaza siku ya Jumapili.

Lakini mratibu wa misaada hiyo kwa njia ya anga wa Umoja wa Mataifa katika eneo hilo alisema kuwa kuongeza usambazaji wa misaada kwa njia ya ardhi ni bora zaidi katika kuwafikia watu takribani mlioni 2.4 wenye uhitaji.

Mashirika ya misaada yanasema ni sehemu ndogo tu ya vifaa vinavyohitajika kukidhi mahitaji ya kimsingi ya kibinadamu vimeruhusiwa kuingia Gaza tangu mwezi Oktoba, wakati Israel ilipozingira Ukanda huo.

Bofya hapa: Ukanda wa Gaza unakabiliwa na mzozo wa kibinaadamu ukiongezeka kwenye eneo hilo lililozingirwa.

Wakati huo wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas ilisema siku ya Jumatatu (Machi 11) kuwa idadi ya watu waliouawa imefikia 31,112 katika vita hivyo vya zaidi ya miezi mitano.