1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yapiga tena kambi Gaza vita vikiingia mwezi wa tisa

7 Juni 2024

Vikosi vya Israel vimeishambulia kwa mabomu kambi ya wakimbizi ya Gaza hii leo, baada ya shambulio jengine baya dhidi ya shule ya Umoja wa Mataifa, wakati vita kati ya Israel na Hamas vikiingia katika mwezi wake wa tisa.

https://p.dw.com/p/4gnf1
Ukanda wa Gaza| Baada ya mashambulizi ya Israel Deir Al-Balah
Wapalestina wakikagua uharibifu baada ya shambulizi la ndege za ISrael katika shule ya ya watu waliopoteza makaazi inayoendeshwa na UN katika Kambi ya Nuseirat, 06.06.2024.Picha: Omar Naaman/dpa/picture alliance

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani shambulizi dhidi ya shule hiyo, na kusisitiza wajibu wa kulindwa kwa majengo ya umoja huo hata katika mazingira ya kivita.

Mashambulizi ya usiku yaliofanywa na vikosi vya Israel yaliilenga shule inayoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa linalshughulikia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, na kuuwa watu wasiopungua 40, wakiwemo watoto 14 na wanawake tisa, na kuwaacha wengine 74 wakiwa wamejeruhiwa.

Katika hafla iliyofanyika jana Alhamisi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Guterres alisisitiza kwamba majengo ya Umoja wa Mataifa hayawezi kulengwa, na yanapaswa kulindwa na pande zote wakati wote, hata wakati wa vita.

Marekani, New York | Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka uwajibikaji kwa mashambulizi dhidi ya vituo vya umoja huo.Picha: Yuki Iwamura/AP Photo/picture alliance

Katika hafla hiyo Umoja wa Mataifa ulikumbuka na kutoa heshima kwa wafanyakazi 188 waliopteza maisha yao wakiwa kazini mwaka 2023, miongoni mwao wakiwemo wanawake na wanaume 135 waliokuwa wanalifanyia kazi shirika la UNRWA, ambao wameuawa katika operesheni za Israel Gaza, tangu Oktoba 7.

Soma pia: Israe: Takriban nusu ya wanamgambo wa Hamas wameuwawa

Wengi waliuawa pamoja na familia zao na katika jamii walizokuwa wanazitumikia.

Katibu Mkuu wa UN alikariri wito wake wa uwajibikaji kwa vifo hivyo. "Wafanyakazi wetu wa UNRWA waliishi na kufa kama wawakilishi wa jumuiya ya kimataifa Gaza, na jumuiya hiyo inastahili maelezo," alisema Katibu Mkuu Guterres.

Katika Baraza la Udhamini, linalotazamana na sanamu ya msichana ambaye mikono yake imeinuliwa, ikielekea ndege inayoashiria "Mwanadamu na Matumaini" -- majina ya waliouawa yalisomwa.

Kwa mujibu wa sheria za taasisi hiyo, kibali cha wanafamilia kiliombwa ili kujumuisha majina ya wapendwa wao katika ibada hiyo.

Shule ya UN iliyolengwa na mashambulizi ya Israel katika kambi ya Nuseirat.
Shule ya UN iliyolengwa na mashambulizi ya Israel katika kambi ya Nuseirat.Picha: Omar Naaman/dpa/picture alliance

Kati ya Januari 1 na Desemba 31, 2023, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliouawa walikuwa kutoka jumla ya nchi 37, wakifanya kazi kwa mashirika 18 tofauti. Walikuwa wanajeshi, polisi na raia.

Marekani yaitaka Israel kuwa muwazi

Hospitali ya Mashahidi wa Al-Aqsa mjini Deir al-Balah, katikati mwa Gaza, imesema watu wasiopungua 37 waliuawa katika shambulio la Alhamisi dhidi ya shule ya UN iliyoko kambi ya Nuseirat.

Marekani ambayo inaipa Israel kiasi cha dola bilioni 3.8 kila mwaka katika msaada wa kijeshi, ilimhimiza mshirika wake kuwa muwazi kikamilifu kuhusu shambulio hilo.

Mashahidi pia waliripoti mashambulizi ya Israel mashariki mwa Deir al-Balah na moto mkali kutoka kwenye magari ya jeshi karibu na kambi ya Bureij, ambapo moto ulikuwa ukiwaka.

Soma pia: Israel yaishambulia Gaza baada ya mpango wa amani kukwama

Jeshi la Israel lilisema "limewaangamiza makumi ya magaidi" mashariki mwa Bureij na Deir al-Balah. Lilitoa picha za wanajeshi wanaoendesha operesheni katika majengo yaliyolipuliwa na mabomu katika mji wa kusini wa Rafah.

Gaza Deir El-Balah | miili ya waathiriwa wa mashambulizi ya Israel.
Ndugu wakiomboleza wakati wa kupokea miili ya wapendwa wao waliouawa katika mashambulizi ya Israel Deir El-Balah.Picha: Omar Ashtawy/ZUMA/picture alliance

Watu sita waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulio la Israeli kwenye nyumba ya familia ya Wafati iliyoko kambi ya Maghazi, kilisema chanzo katika hospitali ya Martyrs ya Al-Aqsa.

Israel inaituhumu Hamas na washirika wake kutumia shule, hospitali na majengo mengine ya kiraia, yakiwemo majengo ya Umoja wa Mataifa, kama maeneo yake ya operesheni, madai yanayokanushwa vikali na kundi hilo.

Marekani yarejesha bandari ya kuhamishika Gaza

Kamandi ya Jeshi la Marekani, CENTCOM, imesema jeshi limeirejesha bandari ya muda kuimarisha uingizaji wa misaada Gaza, baada ya kuharibiwa na dhoruba na kufanyiwa ukarabati katika bandari ya Ashdod ya nchini Israel.

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

Zaidi ya pauni milioni mbili za msaada wa kiutu ziliwasilishwa kupitia bandari hiyo mapema mwezi uliyopita, lakini iliharibiwa na dhoruba ya bahari karibu wiki moja baada ya kuanza kutumika.

Soma pia: Hamas, Fatah kufanya mazungumzo ya maridhiano China

Wakati huo huo, shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa ILO, limesema katika ripoti yake iliyotolewa leo, kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira katika Ukanda wa Gaza kimefikia asilimia 79.1 baada ya miezi minane ya vita.

Katika Ukingo wa Magharibi ambako kunashuhudiwa makabiliano ya mara kwa mara kati ya Wapalestina na Walowezi wa Kiyahudi, asilimia 32 ya wakaazi hawana ajira, huku ikiongeza kuwa kiwango hiki kinaweza kuwa kikubwa zaidi.