UN: Wapalestina milioni 1 hatarini kukumbwa na baa la njaa
5 Juni 2024Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) wamesema katika ripoti yao ya pamoja kwamba viwango vya njaa vinazidi kushuhudiwa huko Gaza kutokana na vikwazo vya uwasilishwaji wa misaada ya kibinadamu na kusambaratika kwa mfumo wa chakula vinavyochochewa na vita vya karibu miezi minane kati ya Israel na kundi la Hamas.
Mashirika hayo yameendelea kuwa hali ni mbaya mno kaskazini mwa Gaza, eneo ambalo kwa miezi kadhaa lilizingirwa na kushambuliwa vikali na vikosi vya Israel.
Licha ya vivuko kadhaa vya ardhini kufunguliwa hivi majuzi katika eneo hilo la kaskazini, lakini havitoshi kutumiwa kila siku na makumi ya malori ya misaada ambayo inahitajika kwa mamia ya maelfu ya watu.
Uvamizi wa Israel katika mji wa Rafah umevuruga pakubwa shughuli za usafirishaji na usambazaji wa misaada katika eneo la kusini mwa Gaza. Misri imekataa kufungua kivuko chake cha Rafah tangu wanajeshi wa Israel walipochukua udhibiti wa kivuko hicho kwa upande wa Gaza takriban mwezi mmoja uliopita, na hivyo kupelekea kuhamishwa kwa shughuli za usafirishaji wa misaada kwenye kivuko cha Israel kilicho karibu cha Kerem Shalom.
Soma pia: Hali ya kibinaadamu yazidi kuwa mbaya Gaza
Jeshi la Israel limesema katika wiki za hivi karibuni, limeruhusu mamia ya malori kuingia Gaza kupitia Kerem Shalom lakini Umoja wa Mataifa unasema imekuwa vigumu kuufikia msaada huo kutokana na hali mbaya ya usalama, na kwamba usambazaji wa misaada hiyo ndani ya Gaza unatatizwa pia na mapigano yanayoendelea, kusambaratika kwa mifumo ya sheria pamoja na vikwazo mbalimbali vya Israel.
Israel yaendeleza mashambulizi Gaza
Mapigano yanaendelea huku mashambulizi ya Israel yakiwa yamejikita zaidi katika eneo la katikati mwa Ukanda wa Gaza ambako Israel imesema imeanzisha rasmi operesheni ya kijeshi. Mamlaka za Palestina zimesema kuwa watu wasiopungua 70 wameuawa eneo hilo kuanzia jana Jumanne. Mpalestina aliyelazimika kuyahama makazi yake Bi Um Fadi Shaafout amesema huku akiwahoji viongozi wa Israel:
"Kwa sasa hatuna makazi, kosa letu nini? Mlituondoa kwenye nyumba zetu, mkidai mnataka kuwatokomeza Hamas na kiongozi wao Yahya Sinwar. Lakini hamjafanya lolote kati ya hayo. Netanyahu, je, unadhamiria kulipiza kisasi kwa watoto na wanawake waliolala? Ni kipi ulichofikia, ni yapi malengo yako?"
Soma pia: Israel yafanya mashambulizi ya anga Gaza
Wakati huo huo vyanzo vya kuaminika vimeripoti kuwa wapatanishi kutoka Marekani, Qatar na Misri wamekutana hivi leo mjini Doha kujaribu kukamilisha mpango wa makubaliano ya usitishwaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka. Qatar imesema hivi leo kuwa pendekezo hilo kwa sasa linakaribia kukamilika kwa kuwa linaelekea kutimiza vigezo vya pande zote mbili.
(Vyanzo: Mashirika)