1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatangaza kufanya operesheni maalum Gaza

21 Januari 2025

Israel imetangaza kile inachokiita operesheni maalum kwenye Ukingo wa Magharibi, huku mkuu wake wa majeshi akijiuzulu kufuatia kushindwa kuzuwia uvamizi wa Oktoba 7, 2023.

https://p.dw.com/p/4pRCt
Israel
Israel imetangaza kufanya operesheni maalum kwenye Ukingo wa MagharibiPicha: Jim Hollander/UPI Photo/IMAGO

Mkuu wa Majeshi wa Israel, Herzi Halevi, ametangaza kuwa atajiuzulu nafasi yake hiyo ifikapo mwezi Machi, kwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali vya habari. Luteni Jenerali Halevi ndiye afisa wa juu kabisa wa jeshi la Israel kujiuzulu kutokana na kushindwa kuyazuwia mashambulizi ya Oktoba 7 yaliyopelekea vifo vya watu zaidi ya 1,000 na wengine 250 kuchukuliwa mateka na wanamgambo wa Kipalestina na kufuatiwa na vita vya miezi 15 kwenye Ukanda wa Gaza 

Tangazo hilo la leo la Halevi linakuja wakati jeshi lake likianza kile ilichokiita kuwa ni operesheni kubwa ndani ya eneo linalokaliwa kimabavu la Ukingo wa Magharibi, ambapo limewauwa watu sita na kuwajeruhi wengine kadhaa kwa mujibu wa maafisa wa serikali ya Palestina. Operesheni hiyo ilijikita kwenye mji wa Jenin, ambao umekuwa ukishuhudia uvamizi na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel na mapigano ya mitaani na wanamgambo kwa miaka kadhaa sasa, hata kabla ya uvamizi wa Oktoba 7. 

Mahmoud Abbas ataja kuwa tayari kuiongoza Gaza baada ya vita

Wizara ya Afya ya Palestina inasema tangu Oktoba 7, 2023, zaidi ya Wapalestina 800 wameshauawa na wanajeshi wa Israel kwenye Ukingo huo wa Magharibi. Muda wote ambapo jeshi la Israel lilikuwa kwenye mashambulizi yake kwenye Ukanda wa Gaza, lilikuwa pia likiendesha mashambulizi kwenye Ukingo wa Magharibi, na miongoni mwa mabadilishano ya wafungwa kupitia makubaliano kati yake na Hamas, wamo pia wafungwa kutokea Ukingo huo.

Magari ya misaada yanaendelea kumiminikaUkanda wa Gaza 

Ukanda wa Gaza
Magari ya misaada yanaendelea kumiminika kwenye Ukanda wa Gaza Picha: Mohamed Abd El Ghany/REUTERS

Kwenyewe Gaza, Umoja wa Mataifa unasema magari ya misaada yanaendelea kumiminika kwenye Ukanda huo mfululizo, ambapo kufikia jioni ya jana, malori 915 yalikuwa yameshambaza mahitaji kwa raia wa Ukanda huo. Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, amesema amejulishwa na wenzake walioko Gaza kwamba malori yote yaliyoingia yamefika salama na hakuna mkasa wowote wa uporaji.

Malori ya misaada yaanza kuingia Gaza

Mkuu wa Huduma za Kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, ameitaja hali kwenye Ukanda wa Gaza kuwa ya uhitaji mkubwa na kwamba wafanyakazi wake wanapambana usiku na mchana kuhakikisha kuwa raia wanafikishiwa chakula, maji, vifaa vya makaazi na huduma nyengine muhimu.

Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa inasema kwamba zaidi ya watu milioni wa Gaza, nusu yao wakiwa watoto, wanategemea misaada hiyo. Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, limeanzisha mpango wa siku wa kuongeza idadi ya vitanda na kuwatuma wahudumu kutoka mataifa mbalimbali kwenda Gaza, ambako Haq anasema Wapalestina wapatao 30,000 wana majeraha yanayohatarisha maisha yao na wanahitaji huduma maalum na za haraka. 

Mpango wa kusitisha mapigano Gaza waafikiwa