Rais wa DRC afanya mabadiliko ya baraza la Mawaziri
24 Machi 2023Hatua hiyo imezusha maoni yanayotofatiana maoni miongoni mwa raia wa Kongo, na hasa kuhusu kuteuliwa Vital Kamerhe kuwa naibu waziri mkuu anayehusika na uchumi na Jean-Pierre Bemba aliyeteuliwa kuchukua nafasi ya naibu waziri mkuu mwenye dhamana ya ulinzi wa kitaifa.
Wanasiasa hao wawili walitarajiwa kuwa wagombea urais kwenye uchaguzi unaopangwa kufanyika mnamo Desemba mwaka huu. Baraza jipya la watu 58, linamjumuisha pia Peter Kazadi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye ni mshirika wa karibu wa rais Tshisekedi.
Soma pia: Tshisekedi amrejesha Jean-Pierre Bemba serikalini
Antipas Mbusa Nyamwisi pia ameteuliwa kuwa Waziri anayehusika na ushirikiano wa kikanda wakati ambapo mwanahabari mkongwe wa michezo Kabulo Mwana Kabulo amepewa wizara ya michezo.
Mabadiliko haya yamefanyika wakati Kongo ikibakiwa na miezi minane kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu na hivyo kuzusha maswali mengi.