Japan yamchagua waziri mkuu mpya Shigeru Ishiba
27 Septemba 2024Japan imepata waziri mkuu mpya leo baada ya chama tawala cha Liberal Democratic, LDP, kumchagua waziri wa zamani wa ulinzi Shigeru Ishiba kuwa kiongozi wake kumrithi Fumio Kishida aliyetangaza mwezi Agosti kutowania tena nafasi hiyo.
Ishiba mwenye umri wa miaka 67 amechaguliwa kwa kura 215 dhidi ya 194 za mwanasiasa anayeegemea sera za kizalendo, Sanae Takaichi, ambaye iwapo angechaguliwa angekuwa mwanamke wa kwanza kuliongoza taifa hilo.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi kwenye mkutano wa chama chake ulifanyika mjini Tokyo, Ishiba ameahidi kufanya kazi kwa ujasiri mkubwa na kuifanya Japan kuwa nchi salama kwa kila raia wake.Waziri Mkuu wa Japan Kishida hatagombea tena uenyekiti wa chama chake
Salamu za pongezi zimeanza kumiminika kutoka kila pembe ya dunia huku mataifa hasimu mfano wa China imesema inalenga kufanya kazi na Ishiba kuimarisha mahusiano yaliyopwaya kati ya Tokyo na Beijing.