Je, kiongozi mpya wa IPCC atakuwa mwanamke?
25 Julai 2023Wakati mwanauchumi wa Korea Kusini Hoesung Lee akimaliza muhula wake baada ya takriban miaka minane ya uongozi katika bodi hiyo ya Umoja wa Mataifa iliyoanzishwa mwaka 1988, sasa mwanamke wa kwanza anaweza kuchaguliwa kuiongoza taasisi hiyo muhimu.
Wanawake wawili ni miongoni mwa wagombea wanne wa nafasi hiyo. Thelma Krug kutoka Brazil, ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa IPCC na mtafiti wa zamani katika taasisi ya anga nchini mwake.
Mwengine ni Debra Roberts wa Afrika Kusini, mwanajiografia aliyebobea katika masuala ya ukuaji wa miji na ambaye kwa sasa ni mwenyekiti msaidizi wa kikundi kazi cha IPCC kinachochunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa jamii na mifumo ya ikolojia.
Wanawake hao wawili wakichaguliwa, watakuwa pia wenyekiti wa kwanza wa IPCC kutoka Afrika au Amerika ya Kusini.
Soma pia: IPCC:kutoa ripoti ya hali ya joto duniani
Mtaalamu wa masuala ya hali ya hewa Valerie Masson-Delmotte, ambaye anaongoza mojawapo ya vikundi kazi vya IPCC, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa ni muhimu kuwa na wagombea wanawake kwenye orodha hiyo, tofauti na mwaka 2015 ambapo wagombea sita wa nafasi hiyo wote walikuwa wanaume.
Masson-Delmotte ameendelea kusema kuwa si kwa sababu wao ni wanawake tu, lakini ni watu wenye ujuzi wa kisayansi wa hali ya juu na ambao wanaelewa vyema misimamo tofauti ya kisiasa na kijamii katika nchi tofauti ulimwenguni, huku akisisitiza kuwa wagombea wote wanne wana maono ya kuleta ari mpya wakati huu wa changamoto lukuki.
Wagombea wengine wawili wanaowania nafasi hiyo yamkuu wa IPCC ni Jean-Pascal van Ypersele raia wa Ubelgiji na mtaalamu wa masuala ya hali ya hewa ambaye hapo awali aligombea pia wadhifa huo mwaka 2015. Mgombea mwengine ni Jim Skea raia wa Uingereza na profesa wa nishati mbadala katika Chuo cha Imperial mjini London. Skea ni mwenyekiti mwenza wa kikundi kazi cha IPCC kinatafakari jinsi ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.
Mkutano wa Nairobi utakuwa mkutano wa 59 wa IPCC ambao pia utashuhudia uchaguzi wa wanachama 34 katika ofisi ya bodi hiyo. Wanachama wa IPCC , ambayo ilishinda Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2007 kutokana na kazi zake, watakutana jijini Nairobi kuanzia Julai 25 hadi 28 ili kumchagua mwenyekiti mpya kati ya wagombea na wanasayansi wanne mashuhuri, wote wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 60.
Soma pia: UN kutoa ripoti ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi
Kwa muda mrefu, usawa wa kijinsia umekuwa changamoto katika ulimwengu wa sayansi ya hali ya hewa. Hadi leo hii, wakuu wote wa IPCC wamekuwa wanaume. Ripoti ya mwaka 2019 iligundua kuwa idadi ya wanasayansi wa kike wanaofanya kazi na IPCC iliongezeka hadi kufikia karibu 30% kutoka kwa asilimia 10% pekee.
Yeyote atakayechaguliwa katika wadhifa huo wa juu atawasimamia na kuwaongoza mamia ya wataalam hadi mwisho wa muongo huu muhimu, unaozingatiwa kuwa fursa ya mwisho kwa binadamu kuchukua hatua mbadala za kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzi 1.5 kipimo cha Celsius, ikilinganishwa na viwango vya kabla ya enzi za viwanda.
Athari za mabadiliko ya tabia nchi zinashuhudiwa ulimwenguni kote. Mwezi Juni umeweka rekodi ya juu ya joto kali zaidi hasa katika maeneo ya kusini mwa Ulaya, Marekani na China kulikoshuhudiwa mafuriko, joto kali, mioto ya nyika, ukame na mafuriko.
Kila baada ya miaka mitano hadi saba IPCC huchapisha ripoti zilizokaguliwa na wanasayansi mahiri duniani, ambazo huweka wazi matukio ya hivi punde ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Ripoti ya hivi majuzi iliyochapishwa mwezi Machi, iliweka wazi kwamba ripoti za hapo awali kwa kiasi fulani hazikuangazia ipasavyo madhara ya ongezeko la joto duniani.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mfululizo wa ripoti za IPCC zilizochapishwa katika kipindi cha mwaka 2021-23 chini ya uenyekiti wa Hoesung Lee wa Korea Kusini, ni ishara nyekundu inayoonyesha hatari inayoikabili sayari.
Ripoti hizo zenye umuhimu mkubwa, huwa kama kiini cha mazungumzo ya hali ya hewa duniani kote, na kutoa mwongozo kwa viongozi wa dunia katika mikutano ya kimataifa ya COP, na kuelezea ni jinsi gani shughuli za binadamu zimechangia katika ongezeko la joto, na jinsi ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na vilevile joto duniani.
Mkutano wa kimataifa wa COP28 utafanyika kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12 mwaka huu huko Dubai.