Je, unajua ni kwanini binadamu hupenda kula nyama?
12 Mei 2022Kwanini wanadamu wanaendelea kwa kiwango kikubwa na ulaji wa nyama?
Wanadamu wamekuwa wakila nyama tangu enzi na enzi, na matumizi yao yamekuwa yakiongezeka kadri miaka inavyosonga mbele.
Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), katika kipindi cha miaka 50 pekee, wameongeza uzalishaji wa kimataifa wa nyama mara nne zaidi hadi kufikia takriban tani milioni 350 kila mwaka.
Na mwenendo huo hauonyeshi dalili ya kupungua. Utabiri wa sasa unaonyesha kuwa FAO itakuwa ikizalisha hadi tani milioni 455 kwa mwaka ifikapo mwaka 2050.
Chanzo cha chakula kisichofaa
Kwa muda mrefu, wanasayansi wameibua wasiwasi juu ya athari ya mazingira kwa chakula hiki kinachopendwa, hasa kuhusu wanyama wanaofugwa katika mashamba makubwa ya kiviwanda, na wamekiona kama chanzo cha chakula "kisichofaa", kwa msingi kwamba kwa uzalishaji wake, kinahitaji nishati, maji na ardhi zaidi kuliko vitu vingine vinavyoweza kuliwa.
Utafiti wa FAO unabaini kuwa uzalishaji wa nyama huchangia kwa asilimia 30 ya jumla ya uzalishaji wa gesi chafu, huchangia kwa asilimia 80 ukataji miti ulimwenguni na hutumia asilimia 70 ya maji safi yanayopatikana ulimwenguni.
Utafiti huo unahitimisha kuwa, kuepuka nyama na bidhaa za maziwa ndiyo njia kuu ya kupunguza athari zetu za mazingira katika sayari hii. Bila matumizi ya nyama na maziwa, matumizi ya mashamba kimataifa yanaweza kupungua kwa zaidi ya asilimia 75.
Saikolojia juu ya ulaji wa nyama
Walakini, watu wengi wanaendelea kula nyama bila kujali. Benjamin Buttlar, mwanasaikolojia wa kijamii katika Chuo Kikuu cha Trier nchini Ujerumani, anahusisha hili na mazoea, utamaduni na mahitaji. Anadhani watu wengi wanafurahia ladha tu. Buttlar ameendelea kusema kuwa mara nyingi, tabia hizi zinawazuia watu kufikiria kuwa ulaji wa nyama ni mbaya kwa sababu ni kitu ambacho wanakifanya kila wakati.
Pia kuna ukweli kwamba kile kinacholiwa hakiwakumbushi watu mateso aliyoyapitia mnyama hadi kutua kwenye sahani.
Hata hivyo, tunapokabiliwa na mtazamo tofauti, iwe katika kuzungumza na walaji wa mboga mboga au kutazama vipindi vya runinga kuhusu ustawi wa wanyama, Buttlar anasema tunaweza kuhisi haja ya kujitetea kwa kusema wanadamu wamekuwa wakila nyama tangu enzi.
Nadharia ya 'nyama ilitufanya wanadamu'
Wanasayansi kwa muda mrefu waliamini kwamba kula nyama kuliwasaidia mababu zetu kustawisha muundo wa miili yao kuwa ya kibinadamu zaidi na kwamba zaidi ya miaka milioni mbili iliyopita, kula nyama na uboho kulimpa mwanadamu wa zamani "Homo Erectus" nguvu anayohitaji kuunda na kuulisha ubongo wake mkubwa.
Lakini utafiti wa hivi karibuni ulihoji umuhimu wa matumizi ya nyama katika historia ya ukuwaji wa mwanadamu. Je, chakula chenye msingi wa mimea kilikuwa na nafasi gani katika historia ya ukuaji wa binaadamu?
Briana Pobiner kutoka Marekani na ambaye anatafiti mabadiliko ya lishe ya mwanadamu, anasema hakuna ongezeko la ukubwa wa ubongo lililoshuhudiwa wakati ulaji wa nyama ulipoanza. Pobiner pia anaamini kuwa mageuzi ya binadamu yanatokana na mchanganyiko wa lishe bora.
Hivi sasa, asilimia 75 ya chakula duniani kinatokana na mimea 12 tu na aina tano za wanyama. Lakini wanadamu wanapotumia sana chanzo kimoja cha chakula, hii inaweza kusababisha matatizo ya kiafya.
Daktari Milton Mills wa nchini Marekani ameiambia DW kuwa, tafiti nyingi zinaonyesha kwamba matumizi zaidi ya protini itokayo kwa wanyama yanahusishwa na aina mbalimbali za saratani.
Nini kinafuata?
Ikiwa hamu ya nyama itasalia kama ilivyo bila kubadilika, itakuwa vigumu kwa idadi kubwa ya watu duniani kuweza kukidhi mahitaji yao ya chakula ifikapo mwaka 2050, wakati idadi ya watu duniani itakapokadiriwa kufikia bilioni 10.
Kilicho muhimu kulingana na Buttlar, ni kuwawezesha watu kuwa na uhusiano mzuri na njia mbadala za kutumia vyakula vitokanavyo na mimea. Mtazamo tayari umeanza kubadilika na sasa unadhihirika.