Je, unamfahamu Giorgia Meloni, mshindi wa uchaguzi Italia?
26 Septemba 2022Georgia Meloni alizaliwa mwaka 1977. Alipokuwa na umri wa miaka 15 alijiunga na mrengo wa vijana wa chama cha Kifashisti mamboleo cha Italian Social Movement ili kudhihirisha msimamo wake dhidi ya ugaidi wa mrengo mkali wa kushoto ambao uliikumba Italia wakati huo.
Baadaye aliongoza tawi la wanafunzi la Muungano wa Kitaifa wa siasa kali za mrengo wa kulia, akachaguliwa katika Baraza la Manaibu wa Bunge la Italia mwaka wa 2006, na kuwa waziri mwenye umri mdogo zaidi wa Italia miaka miwili baadaye.
Akiwa na umri wa miaka 31, Meloni alipewa wizara ya vijana katika serikali ya Berlusconi. Miaka kumi iliyopita, Meloni alianzisha chama cha Ndugu wa Italia, ambacho amekiongoza tangu mwaka 2014.
Mnamo mwaka 2020, Meloni alichukua pia uenyekiti wa chama cha Wahafidhina na Wanamageuzi wa Ulaya ambacho kinajumuisha, miongoni mwa wengine, chama tawala cha Poland, PiS.
Nyota wa siasa kali za mrengo wa kulia
Giorgia Meloni amekuwa nyota wa siasa za mrengo wa kulia nchini Italia. Akitumia kauli mbiu ya "Italia na raia wa Italia kwanza!", Meloni ametoa wito kwa raia kutozwa ushuru mdogo na kusitishwa kwa uhamiaji.
Soma zaidi: Mrengo wa kulia washinda uchaguzi Italia
Anataka pia kujadili upya mikataba ya Umoja wa Ulaya, na chama chake kinapinga uavyaji mimba na ndoa za jinsia moja. Kwa upande wa sera ya uchumi na uhusiano wa kimataifa, Meloni anaonekana kutokuwa na uzoefu. Ametumia muda mwingi wa maisha yake ya kisiasa kama mbunge na afisa wa chama.
Meloni ahusishwa na ufashisti
Wakosoaji wanaonya kuwa Meloni anashabihiana na historia ya ufashisti wa Italia. Meloni mwenyewe hajajitenga waziwazi na ufashisti; katika wasifu wake wa mwaka jana (2021), aliandika kwamba anafahamu kuwa misimamo yake ni yenye utata kisiasa lakini akasema:
" Sisi tumetokana na historia yetu, historia yetu yote. Kama ilivyo kwa mataifa mengine. Tuliyoyapitia ni magumu zaidi kuliko wengi wanavyotaka kuelezea."
Meloni aliwahi kusema katika mahojiano kuwa ana uhusiano thabiti na historia na kwamba Dikteta Mussolini alikuwa "mtu asiyefahamika vyema,". Hadi leo hii, raia wengi wa Italia wanadhani kuwa kila kitu hakikuwa kibaya chini ya uongozi wa Mussolini.
Soma zaidi:Italia yapiga kura kuchagua bunge jipya
Hata hivyo Meloni amepinga suala la kuwa na kiongozi mmoja maridadi kuhusishwa na Ufashisti. Lakini kila mara Meloni anapofanya mikutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama, ishara ya kifashisti ambayo ni nembo ya chama cha Ndugu wa Italia daima hudhihirika wazi.
Meloni amejiandaa kuwa waziri mkuu kwa miaka mingi
Mwanasiasa huyo anataka kukijenga upya Chama chake na kukiondoa kutoka kwenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia na hivyo kuwavutia watu wa tabaka la kati na kuweza kuunda muungano na vyama vingine vya mrengo wa kulia kama kile cha Matteo Salvini na Forza Italia, inayoongozwa na waziri mkuu wa zamani Silvio Berlusconi.
Msimu uliopita, katika maandalizi ya kampeni za uchaguzi wa Septemba 25, Meloni alituma ujumbe kwa vikundi vya chama akiwaagiza waache kutoa kauli kali, wajiepushe kuzungumzia ufashisti na zaidi ya yote, wajiepushe na ile iitwayo salamu ya Kiroma inayofanana na salamu ya Hitler au ya manazi.
Mwanasiasa anayejiamini
Meloni anafahamika kama mwanasiasa mwanamke mwenye kujiamini na asiyeyumbushwa na ukosoaji mkali dhidi yake.
Katika mahojiano kwenye televisheni, Meloni aliwahi kuwaambia wakosoaji wake wazingatie mfano wa Ufaransa na Ujerumani, ambapo vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vimefanikiwa na hakuna aliyegeuza hilo kuwa kashfa huku akihoji kwa nini iwe tofauti nchini Italia?
Alisema pia kuwa, wapinzani wake wamekata tamaa kwa sababu amepata mafaanikio makubwa, na kwamba kumhumhusisha na Mussolini, Hitler au Putin ni ujinga mtupu, kwa sababu hata yeye anaiunga mkono Ukraine katika vita vyake na Urusi.
(DW-English)