Jeshi la sudan na RSF kukutana Jeddah kwa mazungumzo
26 Oktoba 2023Jeshi hilo la Sudan jana lilikubali mualiko wa kushiriki mazungumzo hayo yanayoanza leo likisema hiyo ndio njia mojawapo ya kumaliza mgogoro lakini pia likaweka wazi kwamba bado litaendelea kupigana. Kundi la wanamgambo la RSF nalo pia liliikubali kushiriki lakini muda mfupi baadae likachapisha vidio ya Kamanda wake akiwaaongoza wanajeshi katika eneo la Nyala ambalo ni ngome kubwa ya mapambano.
Licha ya utayari wa jeshi hilo kukaa kwenye meza ya mazungumzo wanadiplomasia na duru za Sudan zinasema watiifu wa rais wa zamani omar al Bashir walio na ushawishi mkubwa jeshini, hawataki mazungumzo na wangelipenda kuendelea kuimarisha ushawishi wao huku mapigano yakiendelea .
Mapigano yaendelea Khartoum licha ya kuwepo kwa mkataba wa usitishaji mapigano
Marekani na Saudi Arabia waliyasimamisha mazungumzo hayo kwa muda, mwezi Juni baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyokubaliwa na pande zote zinazohasimiana kukiukwa mara kadhaa. Lakini kulingana na maafisa wa Marekani, pande hizo mbili sasa zimeamua kuingia tena katika mazungumzo. Afisa huyo amesema miezi kadhaa ya mapigano na mgogoro wa kibinaadamu unaonekana kulemea pande zote mbili.
Duru zinasema jeshi la taifa limekuwa likipambana kurekebisha ndege zake nzee za kivita huku wanamgambo wa RSF wakin'gan'gana kuwapa matibabu wanajeshi wake waliojeruhiwa.
Martin Griffiths asema mapigano yamesababisha mgogoro mkubwa wa kibinaadamu
Umoja wa Afrika na Jumuiya ya kikanda ya ushirikiano wa nchi za Mashariki mwa Afrika,IGAD, watajiunga pia na mazungumzo ya Jeddah, ambayo yatajadili masuala ya misaada ya kitu, kusitishwa kwa mapigano na hatua za kujaribu kupata suluhu ya mgogoro unaoendelea.
Vita kati ya pande hizo mbili vilianza katikati ya mwezi Aprili, kufuatia mipango ya kuijumuisha RSF katika jeshi la serikali, miaka minee baada ya pande hizo mbili kumuondoa rais wa muda mrefu Omar al Bashir. Miezi 18 baada ya hilo kufanyika waliongoza mapinduzi ya kuuondoa utawala wa kiraia uliokuwepo.
Marekani yatiwa wasiwasi na mashambulizi ya RSF
Mapigano yaliotokea tangu muda huo, yamemsababisha mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths, kuyaita mapigano mabaya yaliyosababisha mgogoro mkubwa wa kiutu katika historia ya hivi karibuni, yaliyoharibu mijina maeneo kadhaa ya Sudan, kuwauwa maelfu ya watu na hata kuwafanya watu milioni sita kukosa makaazi yao.
Wanamgambo wa RSF wamedaiwa kutekeleza mauaji ya halaiki Magharibi mwa Darfur.
Chanzo: Reuters