1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Jeshi la Ufaransa laanza operesheni za kuondoka Niger

10 Oktoba 2023

Watawala wa kijeshi wa Niger wamesema msafara wa kwanza wa wanajeshi wa Ufaransa utaanza siku ya Jumanne maandalizi ya kuondoka katika nchi hiyo ya Sahel, baada ya viongozi wa mapinduzi kuwaamuru waondoke.

https://p.dw.com/p/4XLCE
Niger Madama französische Soldaten
Vikosi vya Ufaransa vilivyopo katika kikosi cha Barkhane wakihudhuria sherehe huko Madama karibu na Libya: (01.01.2015)Picha: Dominique Faget/AFP

Taarifa hiyo iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa jana Jumatatu, imeeleza kuwa operesheni za kuondoka kwa msafara wa kwanza utakaosindikizwa na vikosi vya ulinzi na usalama vya Niger, zitaanza leo hii licha ya kuwa taarifa hiyo haikutaja ni wapi msafara huo utakapoelekea.

Taarifa hiyo imeendelea kuwa, kufuatia mikutano kadhaa kati ya mamlaka za Niamey na wawakilishi wa Ufaransa, ratiba ya kuondoka kwa wanajeshi hao imeamuliwa kwa makubaliano ya pande zote.

Mali Unruhen Soldaten
Wanajeshi wa Ufaransa wa kikosi cha Barkhane huko NigerPicha: Sebastien Rieussec/Hans Lucas/IMAGO

Mwishoni mwa juma, kulishuhudiwa misafara kadhaa katika vituo vya kaskazini-magharibi karibu na mipaka ya Burkina Faso na Mali ambako wanajeshi 400 wametumwa, na katika mji mkuu Niamey. Hayo ni kulingana na vyanzo vya usalama vya Ufaransa na Niger.

Angalau misafara miwili imeruhusiwa tena kuendesha zoezi la usambazaji wa bidhaa muhimu kwa vituo vya Ouallam na Tabarey-Barey na wanajeshi kadhaa wa Ufaransa wamepewa vipaumbele kuhamishiwa mjini Niamey.

Soma pia: Vikosi vya Ufaransa vyaanza kuondoka Niger

Wanajeshi wa Ufaransa wamekuwa wakiishi kwa mashaka tangu serikali mpya ilipowataka waondoke, huku wakikabiliwa na matatizo ya ugavi wa chakula na maandamano ya mara kwa mara dhidi ya Ufaransa nje ya kambi ya kijeshi mjini Niamey.

Wanajeshi hao watumia njia gani kuondoka Niger?

	Niger Niamey | Abdourahamane Tiani
Kiongozi mpya wa kijeshi nchini Niger, Jenerali Abdourahamane Tiani.Picha: Télé Sahel/AFP

Njia watakayotumia wanajeshi wa Ufaransa kuondoka nchini Niger bado haijulikani kwa kuwa mipaka ya barabara na mataifa ya Benin na Nigeria imefungwa na utawala wa Niger umepiga pia marufuku ndege za kiraia na kijeshi za Ufaransa kuruka katika anga yake bila idhini maalum.

Hata hivyo Niger imefunguwa tena mipaka yake na Algeria, Libya, Burkina Faso, Mali na Chad, ambako kamandi ya Ufaransa inapatikana katika mji mkuu N'Djamena.

Soma pia:Utawala wa kijeshi wa Niger na kupendekeza mkakati wa kuirejesha nchi hiyo katika utawala wa kikatiba

Kuondoka kwa wanajeshi 1,400 wa Ufaransa kuliamriwa na majenerali walio madarakani nchini Niger, muda mfupi baada ya kunyakua mamlaka kupitia mapinduzi ya kijeshi mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.    

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye alidhamiria kuifanya Niger kuwa mshirika maalum, alisema mnamo Septemba kwamba wanajeshi wake wataondoka "mwishoni mwa mwaka", kwa kuzingatia matakwa ya serikali mpya. Wanajeshi hao wa Ufaransa wako nchini Niger kama sehemu ya mapambano dhidi ya makundi ya itikadi kali za kidini katika eneo lote la Sahel.

Harakati za upatanishi katika mzozo huo

Niger US-Außenminister Antony Blinken mit ehem. Präsident Bazoum
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken (kushoto) akisalimiana na Rais Mohamed Bazoum aliyepinduliwa nchini Niger (16.03.2023)Picha: Presidency of Niger/AA/picture alliance

Alhamisi wiki iliyopita, Nigeria ilipokea vyema ombi la Algeria la kuwa mpatanishi katika mazungumzo na utawala wa kijeshi wa Niger, ambayo yanajumuisha pendekezo la kuwepo kipindi cha mpito cha miezi sita.    

Lakini Algeria imetangaza Jumatatu kwamba "itaahirisha" mazungumzo hayo "hadi ipate ufafanuzi" kuhusu utekelezaji wa upatanishi wake nchini Niger.

Soma pia: Nigeria yapongeza pendekezo la Algeria kuwa mpatanishi Niger

Mapema mwezi huu, viongozi wapya wa Niger walisema muda wa mpito wa kurejea kwa utawala wa kiraia utaamuliwa na mazungumzo "jumuishi ya kitaifa" lakini Kiongozi mpya, Jenerali Abdourahamane Tiani, alisema muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani kwamba kipindi cha mpito kingedumu kwa miaka mitatu.

Hapo jana  Marekani  imetoa wito wa kuachiliwa mara moja wale wote wanaozuiliwa kinyume cha sheria kufuatia mapinduzi ya kijeshi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alifanya pia mazungumzo na rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum na kumhakikishia uungaji mkono kwa utawala uliochaguliwa kidemokrasia katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Vyanzo(AP,RTR,AFP)